30 May 2011

Wabunge waombwa kukomesha biashara ya binadamu

Na Gladness Mboma

BIASHARA haramu ya binadamu na utumwa imedaiwa kushamiri katika mashamba makubwa ya tumbaku yaliyoko katika maeneo mbalimbali yanayolima kilimo
hicho hususan Mkoa wa Tabora, wengi wao wakiwa ni watoto yatima na wanafunzi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Chama cha Kuzuia Matumizi ya Tumbaku Tanzania, Bi. Lutgard Kagaruki wakati akitoa mada kwa Kamati tano za bunge kuhusu athari za tumbaku Tanzania.

"Waheshimiwa wabunge kitu kikubwa kilichotushtua katika utafiti wetu ni juu ya biashara  haramu ya binadamu ambao wanakwenda kuchukuliwa katika nchi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuja kutumikishwa katika mashamba makubwa ya tumbaku Tanzania kwa ujira mdogo,"alisema.

Alisema kuwa watu hao wanakwenda kuchukuliwa katika maeneo ya Masasi, Kagera , Kigoma, Ruvuma na kutoka nje wanachukuliwa katika nchi ya Burundi, ambapo hununuliwa kwa sh. 80,000 hadi 100,000.

Bi. Kagaruki alisema kuwa wengi wa watu hao ni watoto yatima na watu wasiojiweza, wazee pamoja na wanafunzi, ambapo hutumikia malipo kati ya sh. 200,000 hadi 300,000 kwa mwaka.


Alisema kuwa kuna madalali maalumu ambao kazi yao huwa ni kwenda kuwanunua na kuwasafirisha kwa malori hadi katika mashamba hayo na hukatwa gharama za kununuliwa kwao wakati wanapolipwa ujira wao kwa mwaka na wengine hawalipwi.

Alisema kuwa wakati wanapochukuliwa huwa hawajui kama wananunuliwa na hubaini hali hiyo wakati wa malipo kwa kuwa hukatwa fedha kama gharama za kuwanunua.

Bi. Kagaruki alisema  kuwa kutokana na manyanyaso hayo, wengi wa watu hao hawalipwi na pale wanapokuwa wakitaka nauli ya kurudi makwao hupewa mahindi na kisha huambiwa waende kuuza mjini ili kupata nauli ya kurudi kwao, lakini kabla ya kufika mjini hujikuta wakiuawa njiani.

"Tulitaka mjue hali halisi ya nchi hususani katika mashamba yanayolimwa tumbaku na vitu ambavyo viko huko,kwa siku huletwa watu zaidi ya 1,000 na kule wanakotoka wanaandikishiana mikataba ...ninaomba hili jambo mlichukue kwa uzito mkubwa,"alisema.

Alitolea mfano wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Midizimu iliyoko Namtumbo ambaye hakumtaja jina lake amekuwa akifunga shule na kuwapeleka wanafunzi wote katika shamba lake la tumbaku, ambapo hulima kuanzia asubuhi hadi mchana na baadaye kurudi kuendelea na masomo.

Bi. Kagaruki alisema kuwa wazazi wamekuwa wakipiga kelele kuhusiana na suala hilo, lakini, mwalimu huyo amekuwa akiwatolewa vitisho na kuwaambia kwamba hata kama watakwenda kushtaki kwa Rais Kikwete yeye haogopi.

Alisema takwimu za ukataji miti ya kukaushia tumbaku mwaka 2010/2011 iliyotolewa na ofisi ya hifadhi ya misitu mkoa wa Tabora  zinaonesha kwamba jumla ya hekari za miti zilizokatwa kwa ajili ya kukaushia tumbaku ni 56,395  zenye thamani ya sh. 16,712,160,000 na gharama ya upandaji miti hiyo ni sh. 3,136,000,000.

Kwa upande wa wabunge walisikitishwa na biashara hiyo ya utumwa ambapo walimhakikishia Bi. Kagaruki kwamba watakuwa naye bega kwa bega kuhakikisha sheria ya tumbaku ya mwaka 2003 inabadilishwa haraka iwezekanavyo, kwani iliweka mianya ya makampuni ya tumbaku kufanya wanachotaka.

"Kama kweli mnaushahidi wa kutosha ambao unaonesha wapo watu wamechuliwa maeneo mbalimbali wakapelekwa katika mashamba ya tumbaku...inasikitisha kuona biashara hiyo haramu inafanyika na viongozi wapo, nitahakikisha ninashawishi Kamati yangu ya Uvuvi na Kilimo kwenda Tabora kuangalia hiyo hali kwani ni hatari,"alisema Mbunge wa Mafia, Bw. Abdulkarim Shah.

Wabunge hao walisema kuwa kilimo cha tumbaku kimesababisha asali ya Tabora kuanza kukosa soko katika soko la kimataifa kutokana na asali hiyo kudaiwa kuwa na chembechembe ambazo zinatokana na tumbaku hiyo na hivyo kuonekana kuwa na athari kwa walaji.

No comments:

Post a Comment