30 May 2011

Mzumbe yaihakikishia ushirikiano GE

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

CHUO Kikuu Mzumbe kimesema kiko tayari kushirikiana na kampuni kubwa ya nchini Marekani ya General Electric (GE) katika juhudi za kufikia maendeleo
yanayotakiwa Tanzania.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Joseph Kuzilwa amesema chuo chake kinaikaribisha kampuni hiyo ya GE kushirikiana katika kubadilishana ubunifu, mafunzo, utaalam pamoja na kampuni hiyo kuajiri wahitimu wa chuo chake.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe Dar es Salaam, Bw. Andrew Mbwambo, Prof. Kuzilwa alisema chuo
hicho kinashirikiana na wadau mbalimbali toka nchi za Canada, Ulaya na Africa ili kuhakikisha wahitimu wanaotoka chuoni hapo wanafikia viwango vinavyotakiwa kimataifa.

“Hii imefanya wahitimu wetu kuwa na viwango vya juu katika soko,” aliwaambia maofisa wa GE waliotembelea skuli hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Maofisa hao walioongozwa na Rais na Makamu Mwenyekiti mwenye dhamana ya kupanua kazi za kampuni hiyo duniani, Bw. John Rice walikua Tanzania kukutana na wenzao
nchini hapa ili kuangalia fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali kama ya nishati, afya, miundombinu, na usafiri wa anga.

Akiwa katika skuli hiyo, Bw. Rice alisema kuwa kampuni ya GE inatambua fursa za uwekezaji barani Afrika na kusema kwamba Tanzania ina nafasi nzuri ya kushikiana
na kampuni hiyo katika kufanikisha miradi ya maendeleo ya afya, nishati na usafiri katika soko la Tanzania.

Alisema kwa sasa kampuni hiyo imepanga kujiimarisha kibiashara Kusini mwa Jangwa
la Sahara ambalo alisema linatoa fursa kwa ukuaji wa kampuni hiyo kwa muda mrefu ujao.

Akiwa chuoni hapo, Bw. Rice alikutana na wanafunzi na kuzungumza nao kuhusiana na umuhimu wa uongozi bora na maadili katika mazingira yanayobadilika haraka ya
karne ya 21.

Alisema GE inayo teknolojia bora lakini yenye kuhitaji viongozi bora ili kuufanya ujuzi huo kufaidisha nchi zinazoendelea kama Tanzania.

1 comment:

  1. Baada ya kutazama wazungu kwa muda mrefu ni kua hawatoi kitu bila kupata kitu wanachotafuta hapo ni watu wenye vipaji ili wakimaliza masomo hapo wawachukue wakaijenge nchi yao sio Tanzania kama huamini haya ni mambo ya ujanja ujanja tu mchanga wa macho kama vijana wasemavyo lakni yangu macho maana najua nia yao nina ujuzi wa kuyatazama mambo yao kwa miaka 25 sasa tukiwa hai watu watakaosoma maoni yangu watanikumbuka Mzungu hata siku moja hafanyi ila akifanya ni kua anatazama mbali na atapata faida mara dufu ya anachojidai anasaidia ni ukweli ulo wazi lakini kwa kua tuna shida inabidi tukubali

    ReplyDelete