30 May 2011

Viongozi chimbuko la migogoro ardhi-Dkt Shein

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa chimbuko la matatizo ya ardhi katika Mkoa wa Kusini Unguja linatokana na viongozi kutowajibika ipasavyo
katika kuyapa ufumbuzi kwa muda muafaka.

Hayo aliyasema katika Wilaya ya Kati Unguja, wakati akitoa majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo.

“Matatizo ya ardhi ambayo yamekuwa yakitokea katika Mkoa huu yamekuwa yakichangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa Mkoa, Wilaya, Wadi na Shehia pamoja na viongozi wa Wizara”, alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliwasisitiza viongozi kuwasaidia wananchi katika Mkoa huo kwa kuwatatulia matatizo yao ya ardhi na kuwataka kutojiingiza katika mgogoro
huo hivyo wawe mstari wa mbele kuyatafutia ufumbuzi, kutokana na uwezo walio nao kisheria.

Aidha aliwataka viongozi wa Mkoa huo kutokaa maofisini na badala yake wawatembelee wananchi katika maeneo yao kwa lengo la kusikiliza matatizo yanayowakabili.

Dkt. Shein alisema kuwa wananchi wa Mkoa  wa kusini wana matumaini makubwa na serikali yao na kuwataka viongozi hao wa Mkoa wa Kusini kubadilika na kufanya kazi kwa uadilifu na taratibu zote za kisheria zilizowekwa ili
wananchi waendelee kuwa na imani na serikali yao.

Alisema miongoni mwa mambo aliyogundua katika ziara yake hiyo ni pamoja na viongozi wa Mkoa huo kutokuwa karibu na wananchi na hivyo wananchi kukosa
viongozi wa kuwaelezea matatizo yao.

Hata hivyo hakusita kuwataka wananchi wa Mkoa huo wa Kusini kushirikiana na viongozi wao wa Mkoa na Wilaya katika kuendeleza shughuli zao za maendeleo
na kupongeza Halmashauri kwa kuajiri vijana wenye sifa za elimu pamoja na kukusanya mapato makubwa katika Wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment