30 May 2011

SIKIKA; Bajeti Wizara ya Afya haifai

Na Mwandishi Wetu

BAJETI ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya 2010/11 imejaa mipango isiyofaa na isiyozingatia kanuni, uhalisia na ufanisi hali inayoifanya wizara hiyo ishindwe
kufanya kazi zake ipasavyo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na Utetezi kwa ajili ya Huduma Bora za Afya kwa Watanzania wote (SIKIKA) Bw. Irenei Kiria kwenye uchambuzi wa bajeti ya wizara hiyo ya 2010/11.

"Uchambuzi wa Bajeti ya Sekta ya Afya ni moja ya shughuli kubwa za SIKIKA katika kutetea mgao wa bajeti na matumizi yenye ufanisi" alisema Bw. Kiria.

Alisema SIKIKA imechambua mgao wa fedha wa sekta ya afya na kujikita kwenye bajeti ya wizara hiyo za mikoa na kugundua kwamba mipango iliyopo inakinzana kwa kiwango kikubwa na kukumbatia ufanyaji migao maradufu kwa shughuli moja.


Alisema kuwa pamoja na mabaya hayo, SIKIKA inatambua juhudi za wizara hiyo katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, ambapo wizara imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi hayo.

Alisema kuwa migao maradufu imeonekana kuwa shughuli moja inaweza kupangiwa fedha kutoka kwenye vyanzo zaidi ya kimoja.

Alitoa mfano kuwa wakati ni wajibu wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania kulipia safari za wabunge majimboni mwao, Kurugenzi ya Sera na Mipango ya Wizara ya Afya ilipanga kutumia sh. milioni 75 kwa ajili ya safari za Waziri, Naibu Waziri na maofisa wanne kutembelea majimbo yao ya uchaguzi.

Alisema kuwa mgao huo wa fedha haukubaliki hasa ikizingatiwa kuwa kiasi hicho ni zaidi ya mara mbili ya fedha ambazo mikoa hupokea kutekeleza miradi ya VVU/UKIMWI au shughuli za kuzuia maambukizo ya VVU/UKIMWI.

Alisema kuwa mgao kwa ajili ya miradi hiyo kwenye Programu ya Sekta ya Afya ya Msingi ni sh. milioni 30 kwa mkoa.


Mipango isiyozingatia uhalisia Katika bajeti hiyo  iliyochambuliwa, kifungu namba 1005, chini ya kipengele cha Safari za Nje ya Nchi,Wizara imetenga shilingi laki moja tu kwa ajili ya safari hizo lakini, katika hali halisi fedha hizo hazitoshi kwa ajili ya shughuli hiyo.

"Hii inaleta wasiwasi kwamba migao hii haikufanywa kwa umakini; ama sivyo hilo lisingejitokeza kwenye mipango hiyo mipango isiyofaa mmoja wa mifano inayoonesha mipango isiyofaa na isiyo na tija ni ule wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani mwaka huu ambapo sh. milioni 62 zinatarajiwa kutumika.

"Ukweli ni kwamba matumizi hayo yangepunguzwa na kuelekezwa kwenye maeneo yenye tija kama vile ya ununuzi wa vyandarua hivyo kupunguza maambukizo ya malaria,"alisema Bw. Kiria.

Alisema mfano mwingine wa mipango isiyofaa, ni kwamba pamoja na kuongezeka kwa matukio ya saratani nchini, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road haikupata fedha  yoyote iwe ya ndani au nje ya nchi kwenye bajeti hiyo. Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pia haikuambulia chochote.

Bw.Kiria alisema wakati matumizi zaidi ya shughuli za maendeleo kwa ajili ya kupambana na VVU/UKIMWI yanakaribishwa kwenye bajeti hiyo, fedha hizo zimegawanywa bila kuzingatia viwango vya maambukizo ya VVU/UKIMWI. kwakufuata mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha maambukizo ya VVU/UKIMWI.

Alifafanunua kuwa asilimia 16, ya matumizi yake katika shughuli za maendeleo kwa VVU/UKIMWI ni sh.328 kwa kila mtu, wakati Arusha, ambayo ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango kidogo cha maambukizo nchini (2%),inapata sh. 411 kwa kila mtu.

No comments:

Post a Comment