31 May 2011

Tuhuma za rushwa Bavicha zipelekwe TAKUKURU-Zitto

Na Tumaini Makene

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Kabwe Zitto ametoa pongezi kwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Vijana (BAVICHA), huku
akisema kuwa atamwandikia barua katibu mkuu wake, kushauri tuhuma za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa juzi, zipelekwe mbele kwa hatua zaidi.

Akizungumza na Majira jana, Bw. Zitto alisema kuwa leo atawasilisha barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, kumwomba tuhuma za rushwa zifikishwe katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili zifanyiwe uchunguzi, kisha hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika.

"Nafikiri nitaiwasilisha kesho hiyo barua, nitamwomba katibu mkuu hizi tuhuma zifikishwe PCCB, nafikiri hiyo itakuwa ni hatua bora zaidi, PCCB wachunguze watakaobainika na makosa wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wengine wote wanaojihusisha na vitendo vya namna hiyo ndani ya chama.

"Nitatumia nafasi yangu ya Naibu Katibu Mkuu. Kwa sababu tusipofanya hivyo itaweza kujenga hisia za kuwa walioondolewa katika uchaguzi huo kwa tuhuma za rushwa wameonewa. Italeta hisia za upendeleo...kwa sababu mwenye haki ya ku-determine rushwa ni mahakama hivyo ni bora wachukuliwe hatua zaidi," alisema Bw. Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Akizungumzia ushindi wa Mwenyekiti wa BAVICHA, Bw. John Heche, alisema kuwa changamoto kubwa aliyonayo ni kuwaunganisha vijana wote na kuwa kiongozi wao, wakiwemo wale waliokuwa washindani wake na watu waliokuwa nyuma yao wakiwasapoti.

"Nampongeza sana Heche, kwa ushindi wake alioupata. Sasa hivi ni wakati wa kukijenga chama, uchaguzi umeisha si wakati wa kulalama tena...vijana wanamtegemea atakuwa mwenyekiti wao, mimi nafikiri moja ya changamoto zake kubwa ni pamoja na kuwaunganisha vijana, wote hata walioenguliwa," alisema Bw. Zitto.

Juzi akizungumza na Majira juu ya uchaguzi wa BAVICHA uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Slaa alisema kuwa vitendo vyote vilivyo kinyume na maadili ya kampeni kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha katiba ya chama hicho, pamoja na waliohusika, vitajadiliwa katika ngazi ya Kamati Kuu kwa maamuzi zaidi.

Alisema kuwa baadhi ya wagombea, hasa walioenguliwa, walibainika kwenda kinyume na maadili ya chama hicho, hasa katika kupiga vita ufisadi wa aina yoyote kama vile kufanya hila katika uchaguzi, kujenga makundi yenye kuhatarisha chama na kutaka kuvuruga uchaguzi.

6 comments:

  1. "atamwandikia barua katibu mkuu wake, kushauri tuhuma za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa juzi, zipelekwe mbele kwa hatua zaidi"? Kwani huwa hamkai na kuongea mambo yenu? mpaka uandike barua?
    Unategemea PCCB na serikali ya CCM watagundua nini? Kwani hamkuwajulisha kuwa mna uchaguzi ili watume akari kanzu? Unategemea jibu lao litakuwa nini?

    ReplyDelete
  2. Zitto acha undumilakuwili! Utatoweka kwenye anga za siasa za maji taka muda si mrefu. Nami nataka kukupeleka takukuru wachunguze tabia yako ya ufuska kama haina madhara kwa kazi yako ya ubunge na uenyekiti wa kamati

    ReplyDelete
  3. utapompeleka mgombea takukuru halafu unasema aunganishwe ndani chini ya Heche una maana gani?

    attempt za kutafuta ushawishi huwa zipo katika chaguzi zote...zipo zinazojulikana, na nyingine zisizojulikana...ndio maana hata mtu akishindwa uchaguzi kwa tuhuma za rushwa huwa hafungwi??

    Mungu mbariki Heche, Mungu Ibariki Chadema

    ReplyDelete
  4. kaka bw anonymous acha kashfa we shauri juu ya mada iliyombele acha zengwe, vp zitto alikuchukulia dem wako nini maaana umemvaa kimtaani zaidi,

    ReplyDelete
  5. zitto takukuru wapelekwe nini wkt mlisema hawana uwezo wa kuzuia rushwa sasa leo uwezo wamepata wapi? au ndio kujivua gamba kaka watoaji ndy nyinyi mnataka takukuru wa nini? kwn mpk barua uandike nenda takukuru peleka majina km raia mwema .

    ReplyDelete
  6. NI SAHIHI ZAIDI KAMA KWELI MAMBO YA KISHERIA YAKAFUATA MKONDO WAKE , WAONYESHE MFANO MAANA WAMEWASHIKA WAKITOA RUSHWA NA NDIO MAANA WAKAWAENGUA KATIKA KUGOMBEA UONGOZI PIA NA WALE WOTE WALIOKUWA NA VISU KAMA SILAHA BILA LESENI YA KUMILIKI WALISHIKWA NI KUNDI MOJA KUPELEKWA KWENYE MKONO WA SHERIA,. MASUALA YA KUTUIMBIA NYIMBO ZILE ZILE NA MAPAMBIO YALE YALE NADHANI UMEPITWA NA WAKATI, VINGINEVYO WANAIMBA KUTAFUTA KULA NA SIO KUTENDA HAKI NA NI KUNDI MOJA NA WALIOPO MADARAKANI SASA

    ReplyDelete