31 May 2011

Mrema aagiza mweka hazina awekwe kando

Na Gladness Mboma

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeagiza Mweka Hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, Bw. George Kitunga avuliwe wadhifa wake
na kukatwa mshahara kwa madai ya kuingia mikataba ya 'kifisadi' ya ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Augustino Mrema alitoa agizo hilo baada ya Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kujichanganya katika kutoa maelezo kuhusu matumizi ya fedha za halmashauri hiyo wakati walipokuwa waliwasilisha kwa kamati ya bunge.

Halmashauri hiyo ilionekana kujichanganya katika kutoa maelezo kuhusu mapato na matumizi ya fedha yaliyoko katika nyaraka ambazo zilikuwa zinasomwa na Mkaguzi wa Mahesabu za Serikali Kanda ya Kaskazini, Bw. Asalea Kihupi, hali ambayo ilizua maswali mengi kwa kamati ya bunge.

Kutokana na mkanganyiko huo, Kamati hiyo iliamua viongozi hao kutoka nje kwa muda, na walipoitwa, yalitolewa maazimio ya kumvua wadhifa Bw. Kitunga na kubadilishwa kwa kitengo chote cha fedha.

"Kwa kifupi kamati haijaridhika na kazi ambayo ilitakiwa kufanyika, leo vitabu vina dosari kubwa na tumeona kuwa tukianza kuwahoji na kuwakagua tunapoteza muda wetu, inaelekea hamjajiandaa kuja kwenye kamati hii leo, ninyi ni wazembe na inaelekea hamfanyi kazi zenu kwa umakini," aliwaeleza Bw. Mrema.

Alisema kuwa vitu ambavyo kamati ilihitaji kama nyaraka za miradi ambazo walitakiwa kukagua hazipo, na nyingine zilizopo si sahihi, hivyo wasingeweza kuwatendea haki wananchi wa Halmashauri ya Arusha kwa kukagua nyaraka hewa.

"Kuna watu lazima waadhibiwe hatuwezi kunyamaza, Mweka hazina atakuwa ndiye mtu wa kwanza kuadhibiwa kwa kuifikisha halmashauri hapo ilipo kwa kushindwa kuthibitisha vitabu vya fedha vilipo," alisema.

Alisema kuwa kwanza kamati imeamuru mshahara wake kukatwa, ambapo pia imemwamuru Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw Estomy Chang'a kuhakikisha anamwandikia barua ya kumuondoa katika kitengo hicho pamoja na kitengo chote cha fedha.

Bw. Mrema alisema kuwa kitengo hicho kinatakiwa kufanyiwa marekebisho na kisiachwe kama kilivyo na badala yake achaguliwe mweka hazina mwingine ambaye ni mwaminifu atakayefanya kazi hiyo.

Alisema kamati hiyo itakwenda kuzungumza na waziri pamoja na Katibu Mkuu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusiana na suala hilo.

Alisema kuwa mikataba mibovu ambayo viongozi hao wameingia imeisababishia halmashauri hiyo hasara ya sh. bilioni moja, kisha akaamuru kila mbunge awarudishie mahesabu viongozi hao huku akiwataka wasihesabu kwamba walikuwa kazini jana bali walikuwa Dar es Salaam kufanya manunuzi, kwa kuwa kazi yao aina viwango.

"Kamati imependekeza kwamba kuanzia sasa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha amwandikie barua mweka hazina ya kumshusha cheo alichonacho na apewe kazi nyingine wakati anawasilisha barua TAMISEMI" alisema.

Naye Mbunge wa Rombo, Bw. Joseph Selasini alisema kuwa mweka hazina huyo anatakiwa kusimamishwa mara moja na kutafutwa mtu mwingine na kumtaka mkurugenzi kutofanya kazi na mtu ambaye hana imani naye wakati fedha za serikali zinapotea.

"Usisubiri TAMISEMI ndipo umvue cheo, mwandikie barua kuanzia sasa, hadi TAMISEMI watoe hiyo barua ni lini?  Tekeleza ili agizo wakati TAMISEMI inaandaa barua ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho katika kitengo cha uhasibu," alisema.

Alisema kuwa kamati haiwezi kuona fedha za halmashauri zinaendelea kuteketea na badala yake wanataka mhusika asimamishwe, kwa amriya kamati hiyo.

Naye Kaimu Meya wa Halmashauri hiyo ya Arusha, Bw. Gaudencia Lyimo alisema kuwa amefurahishwa na kamati hiyo, kwani ni makini na ndiyo itakayoleta maendeleo ya kweli.

"Mimi binafsi sitopenda kuona mapato na matumizi ya halmashauri yangu yakienda vibaya, uamuzi uliochukuliwa mimi ninaunga mkono, kwani tumekuwa tukipigia kelele kwa muda mrefu. Nadhani leo imefikia mwisho wake hata kama wapo watakaochukia nilichosema, lakini huu ndio ukweli mapato Arusha yanapungua siku hadi siku," alisema.

Awali Bw. Chang'a aliiambia kamati hiyo kwamba uwezo wa halmashauri hiyo kukusanya mapato kufikia lengo katika kipindi cha mwaka 2008/2009 umeshuka kwa kasi kutokana na mawakala ambao waliwapa zabuni za kukusanya mapato kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Bw. Chang'a alisema kuwa pia tatizo hilo la ukusanyaji mapato limetokana na udhaifu wa vipengele vilivyoko katika mikataba yao na kwamba wanatarajia mwaka ujao wa fedha mapato yatapanda.

Alisema kuwa mapato yameshuka kutoka sh. bilioni 22 hadi kufikia sh. bilioni 17 katika kipindi cha mwaka 2009/2010, ambapo Bw. Selasini alitaka kujua aliyehusika na mikataba hiyo mibovu na hatua alizochukuliwa.

4 comments:

  1. Hongera Mrema kwa kazi yako nzuri unayofanya. Kwa stail hii nadhani kila Halmashauri itakuwa makini kutokana na umakini na uwajibishaji wa Kamati yako kwa maamuzi inayotoa kutokana na Baadhi ya viongozi kutokuwa makini

    ReplyDelete
  2. Sawa Lyatonga na kamati lakini mnafuatilia maagizo yenu? angalieni usije ukamkuta huyo jamaa hapo hapo nafasi ileile anadunda! Au wakampeleka halmashauri nyingine yenye ulaji zaidi! Fuatilieni si kutoa maagizo halafu mnatimka! Hakika bila kubana hizi halmashauri maendeleo TZ yatakuwa ndoto ya alinacha

    ReplyDelete
  3. Lakini ngoja tujiulize, mbona IKULU, TAA KUU KUU (TAKUKURU) na GESHI LA POLISI kimyaaa! hapa si ndio angalau wangesafisha jina? Ushahidi nje nje hata wahusika wanakiri wizi upo! Mkuu wa kuivua gamba mbona kimya? Mzee wa intelijensia viiipi? Na huyo KOSEA (HOSEA) wa WikiLeak mbona zii? Au na hapo umetishiwa na MKUU? Acheni hizo, kamateni wezi tupate maendeleo. Hivi mnafurahia nini nchi kukosa maendeleo? Mnakera kuliko uharo wa mmasai!

    ReplyDelete
  4. Kweli kabisa ndg. Anonymous hapo juu. Hawa viongozi wanakera kweli. Halafu ni kama wanatufanya watanzania mabwege fulani hivi?? Mambo yanaeleweka halafu hatua hakuna; inashangaza kweli?? Ushahidi uko wazi, mtumishi anaachwa kujivinjari tu bila tabu yeyote. Angalia, hivi karibuni Waziri Membe ametukuna watanzania kwa kutetea "Chenji" ya Rada toka Uingereza kurudishwa serikalini badala ya kuipa taasisi isiyo ya kiserikali, hapo sawa kabisa. Lakini hasemi juu ya hatua yeyote itakayochukuliwa dhidi ya waliyolipa hiyo ziada ya fedha!!! Mmmmmmh!! Takukuru wapo, Ikulu kimya, Polisi ndiyo kabisa imelowa maji?? Ingalikuwa kajambanani mmoja hapo, ungaliona kasheshe anayofanyiwa. Takukuru wamebaki kutega mitego ya kuwanasa mahakimu na mapolisi kwa kuwapa fedha za "Moto" yaani wanatafuta makosa yaliyojificha. Ujinga gani huu?? Mafisadi papa na nyangumi wanaachwa?? Stupid!!! Inaudhi sana tena sanaa.Tunaomba kujua, hivi waliohusika na bei haramu ya rada (Mkapa, Chenge n.k. wanachukuliwa hatua zipi???

    ReplyDelete