Na Benjamin Masese
AGIZO la Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omari Nundu kumuagiza Mkurugenzi wa Tazara Bw. Akashambatwa Mbikusita kuhakikisha anawalipa wafanyakazi mshahara
ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi limeshindikana mwamba baada ya kushindwa kutekelezwa na kusababisha wafanyakazi kusitisha shughuli zote na kuvamia ofisi yake kudai haki yao.
Wafanyakazi hao walifika ofisini hapo jana saa tatu asubuhi na kuzingira jengo hilo huku viongozi wao wakiingia ndani kuonana na mkurugenzi huyo na kufanya nao kikao cha dharura.
Hata hivyo, uzalendo uliwashinda wafanyakazi hao kusubiria majibu kutoka kwa wawakilishi na hatimaye kuvamia ofisi hiyo kitendo kilichofanya kikao kusitishwa kwa muda ambapo viongozi wao waliowamba kutoka nje ili kuwaeleza kilichojiri.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli ya Tazara Makao Makuu (TRAWU), Bw. Benjamin Kehogo alisema kuwa mkurugenzi huyo kwenye kikao amedai kuwa ameagiza fedha za makusanyo ya wiki iliyopita katika vituo mbalimbali kuingizwa kwenye akaunti ya Tazara kwa lengo la kuwalipa.
Alisema kuwa fedha zinazosubiriwa kuingizwa kwenye akaunti ni dola laki tano za Marekani na kati ya hizo dola laki mbili zitatumwa kuwalipa wafanyakazi wa Zambia.
Hata hivyo wafanyakazi walisema kuwa bila kupewa mshahara hawataondoka katika ofisi hiyo huku wakitishia kusitisha safari za treni kuondoka hapo kituoni.
Naye Msemaji wa Tazara, Bw. Conrad Simuchile alisema kuwa ingawa ni kweli wafanyakazi wanadai mshahara wao wa Aprili lakini pia wana lengo binafsi la kutaka mkurungenzi wa Tazara kuondoka.
Bw. Simuchile alisema menejimenti inafanya mikakati ya kuwalipa mishahara yao na kuongeza kuwa wamefanya makubaliano na benki moja ambayo hakutaka kuitaja ili kuwalipa wafanyakazi kila mwezi.
Hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omari Nundu aligeuka kuwa 'mbogo' kwa menejimenti ya TAZARA, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU) na wafanyakazi kwa ujumla baada ya kumuita kuwatatulia matatizo yaliyo chini yao ikiwemo mishahara kitendo kilichomkera na kuwapa mwezi mmoja kukaa pamoja na kumpatia taarifa ya utekelezaji.
No comments:
Post a Comment