Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi (Maproo), Nizar Khalfan, Abdi Kassim 'Babi' na Dan Mrwanda wataukosa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu ya
Taifa 'Taifa Stars' na Afrika Kusini 'Bafana Bafana' kutokana na kunyimwa ruhusa na klabu zao.
Nizar ambaye anakipiga Klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada, amenyimwa ruhusa kutokana na timu yake kuwa na mchezo muhimu Mei 15, mwaka huu wa ligi kuu ya nchi hiyo.
Babi na Mrwanda ambao wanakipiga Vietnam katika Klabu ya DT Long, wataisaidia timu yao kupigania kutoshuka daraja katika ligi kuu ya nchi hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema wamchezaji wengine wa wanaokipiga nje kama Idrissa Rajab, Henry Joseph na Athuman Machupa bado wanafuatilia majibu katika klabu zao.
"Hatuwezi kufanya lolote kwa wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi endapo wasipokuja katika mchezo huu, kwani ni ambapo haupo katika kalenda ya FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu), hivyo ni hiari yao kuwaruhusu au kutowaruhusu," alisema Wambura.
Alisema kwa upande wa Taifa Stars, maandalizi yanaendelea vizuri kwani walianza kambi tangu Mei 7, mwaka huu na wachezaji wote wapo katika hali nzuri.
Wakati huohuo, Wambura alisema kikosi cha Bafana Bafana kinatarajiwa kutua nchini kesho jioni kikiwa na msafara wa watu 30, 20 kati yao ni wachezaji ambao wataongozwa na nahodha ambaye ni kiungo wa Kaizer Chiefs, Siphiwe Tshabalala.
Alisema wachezaji wengine watakaowasili na kikosi hicho kinachofundishwa na Kocha Pitso Mosimane ni makipa: Itumeleng Khune na Wayne Sandilands.
Aliwataja mabeki kuwa ni Morgan Gould, Siyanda Xulu, Eric Matoho, Mzivukile Tom, Prince Hlela, Siyabonga Sangweni, Tefu Mashamaite na Siyanda Zwane.
Wambura alisema wachezaji wa viungo waliofuatana na timu hiyo ni Hlompho Kekana, Thanduyise Khuboni, Reneilwe Letsholonyane, Thandani Ntshumayelo, Thabo Matlaba, Erwin Isaacs na Sifiso Myeni wakati washambuliaji ni Bernard Parker, Vuyisile Wana, Lehlohonolo Majoro na Katlego Mphela.
Ofisa huyo aliongeza, tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa kesho,
katika vituo vya Premier Betting kilichopo Kariakoo-Mtaa wa Sukuma, Buguruni Sokoni,
Manzese Midizini, JM Mall, Tandale kwa Mtogole, Shule ya Sekondari Benjamin
Mkapa, Steers (Mtaa wa Ohio na Samora), Big Bon Msimbazi (Kariakoo) na Uwanja wa
Uhuru.
No comments:
Post a Comment