11 May 2011

Bilal azitaka nchi tajiri kutimiza ahadi

Na Mwandishi Maalumu, Instabul

TANZANIA imetoa wito kwa nchi tajiri kutambua nafasi yao katika kuzikwamua nchi maskini ili ziweze kukuza uchumi wake na kuwasaidia wananchi waliomo katika
nchi hizo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohamed Gharib Bilal wakati akihutubia mkutano
wa nne wa Umoja wa Mataifa unaojadili maendeleo ya nchi maskini
unaofanyika nchini Uturuki.

Dkt. Bilal alisema mataifa maskini yametekeleza mambo mbalimbali ambayo
yameshauriwa na mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa, lakini
kikwazo kimebakia katika nafasi za mataifa makubwa kutimiza ahadi zao ili
kuzikwamua nchi maskini kutoka katika hali zilizomo.

"Kama ripoti mbalimbali zinavyoonesha, utekelezaji wa malengo
yaliyowekwa kwa muongo wa mwaka 2001-2010, nchi maskini zimemudu kutimiza
malengo yao mengi, kama sio makubaliano yote yaliyotolewa na nchi tajiri
kwa nchi maskini. Jambo linalokatisha tamaa ni hali ya nchi tajiri
kutotimiza ahadi wanazotoa," Dkt. Bilal alisema.

Akichukulia mfano wa nchi yake, Dkt. Bilal alizielezea nchi wanachama wa
Umoja wa Mataifa kuwa tangu kupitishwa kwa Azimio la Brussels mwaka 2001,
Tanzania ilibadili sera zake nyingi zikiwemo zile zilizolenga kupunguza
umaskini nchini na kuweka mikakati kama MKUKUTA, ikaweka vyombo vya kusimamia ukuzaji wa uchumi, ikaongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya maamuzi, ikaanisha chombo cha kupambana na rushwa huku pia ikitoa uhuru mkubwa kwa vyombo vya habari.

Dkt. Bilal aliendelea kufafanua kuwa, Tanzania katika kipindi hicho
imeongeza uwazi katika mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali,
imefanikiwa kupitia upya mikataba ya madini na imefanikiwa kwa kiwango
kikubwa kutumia uwezo wake wa ndani kutanua wigo wa demokrasia nchini.

Mifano mbalimbali ya Dkt. Bilal aliyokuwa akiitoa katika hotuba yake
ililenga kuonyesha nafasi ya nchi maskini katika kujikwamua lakini
akasisitiza kuwa jitihada hizo peke yake hazitoshi kwa kuwa nchi tajiri
ndizo zinazodhibiti uchumi wa dunia, huku pia zikiwa na fursa nyingi
katika ushindani kuliko nchi maskini.

"Bado ipo haja kwa nchi maskini kupewa fursa zaidi katika soko ambalo
halina masharti magumu. Kama hoja hii ikitekelezwa vema ni wazi nchi hizi
zitamudu ushindani katika biashara za ndani na zile za kimataifa. Hali
iliyopo sasa haitoi fursa hizo," alisema na kuongeza;

"Ili nchi maskini zimudu kuondoka katika kundi hili ndani ya kipindi cha
miaka kumi ijayo, jukumu lililo mbele yetu ni moja ambalo ni kuweka
mikakati ya wazi na kila upande kutimiza wajibu wake kama ambavyo Tanzania
imedhamiria kufanya."

Dkt. Bilal yuko jijini Instabul akiongoza ujumbe wa Tanzania unaohusisha pia wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia sambamba na wafanyabiashara. Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuhusisha wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia na wafanyabiashara katika mkutano wake wa kujadili
maendeleo ya nchi maskini tangu kuanza kwa mikutano hii miaka 30
iliyopita.

No comments:

Post a Comment