05 May 2011

Shein adaiwa kuwalinda mafisadi

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

VYAMA vitatu vya upinzani vimesema Rais Dkt. Shein anawalinda mafisadi wanaotuhumiwa kuuza majengo yaliyomo katika hifadhi ya Mjikongwe kinyume na
sheria.

Tamko hilo wamelitowa kufuatia kauli ya Rais Dkt. Shein kudai serikali haikuwa na ulazima wa kutangaza zabuni katika uuzwaji wa majengo hayo, kwa sababu imeuza mali yake.

Wakizungumza katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo viongozi wa vyama hivyo TADEA, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wakulima (AFP), wamesema mkataba huo uvunjwe ili kulinda sheria namba 9 ya mwaka 2005 ya ununuzi wa Mali za Serikali.

Katibu Mkuu wa TADEA, Bw. Juma Ali Khatib alisema kwamba Serikali ni ya wananchi na mali inayouzwa ni ya Wazanzibari wote na haikuwa muafaka kukodishwa miaka 99 bila kutangazwa zabuni, kama masharti ya sheria yanavyoelekeza.

“Rais alikula kiapo kuwa atalinda katiba na sheria, na mawaziri wake pia walikula kiapo inakuaje serikali inashindwa kuheshimu sheria za nchi,” alisema Katibu huyo.

Alisema kwamba nchi inaendeshwa kwa kuzingatia katiba na sheria na majengo hayo yalistahili kutangazwa zabuni badala ya kuuzwa kienyeji kwa vile sio majengo ya mtu au Ikulu, ni mali ya Wazanzibari wote.

Hata hivyo, alisema kwamba imefika wakati Wazanzibari wakafahamu haki zao za msingi za kikatiba ili kuepusha tabia ya mali za serikali kuuzwa bila ya kuzingatiwa taratibu za sheria.

Naye Mwenyekiti wa AFP, Bw. Said Soud alisema inashangaza Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeshindwa kusimamia misingi ya utawala bora kwa vitendo tangu kuundwa kwake Novemba mwaka jana.

Alitoa mfano alisema sheria za kazi zinasema mtu atastaafu kwa lazima baada ya kufikisha umri wa kati ya miaka 50 na 60, lakini badala yake watu waliostaafu na kulipwa mafao yao wamerejeshwa tena katika utumishi wa umma.

Aidha alisema kwamba hivi karibuni Chama cha Wanasheria Zanzibar, kimekuwa kikilalamika kuhusu uteuzi wa majaji uliofanywa bila ya kuzingatia maamuzi ya tume ya utumishi na maadili.

Alisema kwamba kwa kuwa serikali imeshindwa kuzingatia utawala wa sheria hakuna sababu ya kuwa na Baraza la Wawakilishi na badala yake livunjwe kutokana na serikali kushinda kuzingatia sheria zinazotungwa na baraza hilo.

“Katiba ya nchi inasema mamlaka ya kuendesha nchi ya wananchi wenyewe, tunashauri rais avunje Baraza la Wawakilishi badala ya kupoteza fedha kwa kutunga sheria zisizozingatiwa na serikali,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Dkt. Shein katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar juzi baada ya ziara yake ya Uturuki, alisema kuwa serikali haikufanya makosa kuuzwa majengo hayo bila kutangaza zabuni kwa vile mali iliyouzwa ni ya serikali.

“Serikali haifanyi makosa, ina uamuzi wake hasa kwa mali zake hakuna anayeweza kuhoji, tukiamua kuuza jengo tutauza, Mambo Msiige ni ya Serikali hatujauza mali ya mtu,” alisema Dkt. Shein.

Tangu kuuzwa kwa majengo hayo Oktoba mwaka jana na Serikali ya Awamu ya Sita wanaharakati na wanasheria Zanzibar, wamekuwa wakidai majengo hayo yameuzwa kinyemela kwa dola za Marekani milioni 1.5, bila ya kutangazwa zabuni.

8 comments:

  1. hee Dr Sheni usije ukauza Ikulu bila ya kututaarifu.

    Nakubaliana na mwandishi kwamba Baraza la Wawakilishi livunjwe kwa vile halina maana kupitisha sheria zisizo na mpango. Badala yake Dr Sheni mwenyewe na wenye uwezo serikalini wawe wanajiuzia mali za serikali kila wanapopenda.

    ReplyDelete
  2. Toka lini serikali ikawa inajifanyia mambo kiholela? hakuna serikali yoyote duniani wanaouza au kununuwa kitu chochote bila ya kutowa tenda!! inatolewa tenda,wenye kutaka kununuwa wanatia dau lao, kila mmoja kwa siri kubwa na iliokubaliwa ndio inapata kununuwa mali hio!! pia na kununuwa pia njia ndio hio!! na hii ndio sheria inayokubalika ulimwengu mzima! Vipi hii leo Muheshimiwa Shein aseme kuwa mali hio ni yao serikali? kwani serikali ni ya nani? kama si ya wananchi ambao wameichaguwa hio serikali yenyewe ??????

    ReplyDelete
  3. huyu mtu ana jeuri ya ajabu - typical kiburi cha ccm. wao wanafikiri hii nchi ni ya chama tawala na siyo ya watu. angalia mzozo unaoendelea kule moshi sasa hivi juu ya hawa jamaa walivyojitwalia mali za umma wakazifanya za chama. ubabe una mwisho na anguko la ccm is in sight. viva nguvu ya umma!

    ReplyDelete
  4. Maalim Seif upo kweli?,mbona kimya hivyo au ndiyo umakamu wa Rais MTAMU hivyo,maana ninavyokujua mimi saizi ungekuwa umeisha ita waandshi wa habari kutoa msimamo wa cuf,juu ya uuzwaji wa mali za wananchi kiholela,likini MZEE MADEVU KIMYAAAA,ama kweli madaraka matamu,naamini maneno ya CHADEMA kuwa cuf ya sasa siyo tuliokuwa tunaijua hapo awali,hakuna NGANGARI WALA NGUNGURI,SASA hivi ni Cuf "KONDOO" KUMBE wakina Mboe waliona mbali!

    ReplyDelete
  5. Nyote mmenunuliwa na Aghakhan kwa vile ana bifu na Kempinski basi na nyie ndio mmejitia kati kushabikia ugomvi msioujua! HII NCHI YA MAPINDUZI mmesahau? si ya uhuru kama Tanganyika

    ReplyDelete
  6. Zikowapi ahadi za Shein za kuifanya Unguja na Pemba New York yapili? Maalim Seif, hebu jitikise kidogo kwani tunaona mambo yanakwenda kinyume na matarajio yetu.

    ReplyDelete
  7. Maalim Seif si alisema tokea mwanzo kuwa yupo tayari kufanya kazi na huku Shein awe kiongozi wake? Msione ajabu kwasababu sasa ndio anatimiza ahadi alizozitoa. Seif kakamata makali na mpini umekamatwa na Shein, kwahivo akivuta kisu kitamkata. Au sio?

    ReplyDelete
  8. Ukali wa mwisho wa Maalim ni pale alipoamrisha polisi kuwakamata na kuwachukulia hatuwa waliowacharanga mapanga wana CUF kule sehemu za Bububu katika uchaguzi mdogo baada ya uchaguzi mkuu na kutaka kujuulishwa hatuwa zilizochukuliwa dhidi yao na baada ya hayo hakusikilizana tena. Huenda kaamrishwa kutokujaribu kukitikisa kibiriti

    ReplyDelete