Na Suleiman Abeid, Shinyanga
BAADHI ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na sasa wanalazimika kutumia pumba za mahindi kwa kuzichanganya
katika mahindi na kuzisaga kwa lengo la kupata unga mwingi wa kutosha katika familia zao.
Hali hiyo imebainishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga kilichofanyika juzi mjini hapa ambapo madiwani hao waliiomba serikali ipeleke haraka msaada wa chakula kwa wakazi wa manispaa hiyo kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Diwani wa Kata ya Ibinzamata, Bw. Daniel Mathemu alisema wapo wakazi wa manispaa hiyo ambao wamekuwa wakichukua pumba na kuzichanganya na mahindi na kusaga na kupata unga kwa ajili ya chakula.
Bw. Mathemu ambaye anamiliki vinu vya kukoboa na kusaga nafaka katika eneo la viwanda lililopo kata ya Ibinzamata alisema hali hiyo ya wananchi kulazimika kutumia pumba inatokana na uhaba wa chakula unaowakabili wakazi wengi katika manispaa ya Shinyanga huku wakikabiliwa na ukosefu wa fedha.
Alisema serikali mara nyingi imekuwa ikiwaona wakazi wa maeneo ya mijini kwamba hawana tatizo la uhaba wa chakula kwa vile inaamini wengi wao ni wafanyakazi na wafanyabiashara wakubwa dhana ambayo ni potofu kutokana na wananchi hao kutokuwa na ajira wala uwezo wa kujiajiri.
“Mheshimiwa mwenyekiti, hali ya uhaba wa chakula katika manispaa ni kubwa kulikoni inavyofikiriwa na watu wengi, leo hii ninapoongea hapa mahindi katika mji wetu yameadimika, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la bei ya unga madukani, sasa hivi unauzwa kati ya sh 750 hadi 800/- kwa kilo moja,”
“Hali ni ngumu sana, kama hali itaendelea hivi nafikiri kuanzia wiki ijayo bei itafikia sh. 1,000 kwa kilo moja ya unga, hata bei ya mchele imeongezeka, leo hii (juzi) kilo moja ya mchele inauzwa sh. 1,500 kwa kilo moja, ni muhimu serikali ikaliona hili kwa kutupatia msaada wa chakula mapema,” alieleza Bw. Mathemu.
Kutokana na hali hiyo madiwani hao walikubaliana kwenda kukutana na mkuu wa wilaya ili kumwelezea hali halisi inayowakabili wakazi wa Manispaa ya Shinyanga ambapo wamesema iwapo msaada hautapatikana haraka, wakazi hao watakuwa katika wakati mgumu kutokana na ukame mkubwa uliojitokeza mwaka huu.
No comments:
Post a Comment