05 May 2011

Mwanafunzi akatwa mkono tukio la wizi

Na Theonestina Juma,Bukoba

MTOTO Bonfasi Sijaona mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kasenda Kata ya Muganza Wilayani Chato,amekatwa mkono wa kushoto kwa
tuhuma ya wizi.

Tukio hilo limetokea Aprili 30, mwaka huu, usiku katika Kisiwa cha Chakazimbwe wilayani humo. Kwa mujibu wa habari zilipatikana Mjini Bukoba na kuthibitishwa na Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dkt. Pius Buchukundi mtoto huyo alikatwa mkono huo hadi kubaki ukining'inia.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo watu waliompiga hadi kumkata mkono wake walimkuta ndani ya banda la kuuzia simu za mkononi usiku baada ya kutumwa na wajomba zake watatu.

Alisema watu hao asiowafahamu majina yao walipofika, wajomba zake hao walikurupuka kwa mbio ambapo wakati huo tayari walishabomoa sehemu ya banda hilo, tayari kuanza kazi za kutoa bidhaa zilizokuwemo na kuzipitisha kwenye tundu.

Alisema siku ya tukio wajomba zake hao walimtoa kwao Kasenda na kwenda naye katika kisiwa hicho kwenda kumsalimia shangazi yake.Alisema wajomba hao wamekuwa wakimtumia katika masuala ya wizi na kumlipa sh.2000 kwa kila tukio la wizi anapofanikiwa.

Aliwataja wajomba zake hao kuwa ni pamoja na Revocatus Chibuga,Peter Chibuga na John Chibuga. Mtoto Sijaona alisema baada ya watu hao kumkuta ndani ya banda hilo walianza kumpiga huku akilia kuwa ametumwa hali iliyofanya mtu mmoja kunyanyua panga na kumkata mkono.

Hata hivyo, Dkt. Buchukundi alisema anajaribu kuangalia kama mkono wake unaweza kuunganishwa. Kwa sasa mtoto huyo yuko chini ya uangalizi na atatoa taarifa baadaye kama mkono huo umeshindikana na kuhitaji kukatwa.

1 comment:

  1. DAAH BINADAMU MAKATILI.....HIVI MTOTO WA DARASA LA TATU UNAMKATA MKONO??

    ReplyDelete