10 May 2011

Pentekoste yaionyooshea kidole serikali

Na Benjamin Masese

MAASKOFU, wachungaji na wainjilisti wa madhehebu ya Kipentekoste wameitaka serikali 'kurudisha hisia nyuma na kuona machungu wanayopata wananchi kwa ugumu wa
maisha' huku kukiwa na raslimali nyingi zikiwanufaisha watu wachache wa ndani na nje ya nchi.

Wamesema tatizo lililopo kwa viongozi wa sasa ni kumiliki mzigo wa madaraka, mali na utajiri kwa manufaa ya familia zao huku wakisahaukuwa  mzigo wao mkubwa ni wananchi waliowachagua ili wawaletee maendeleo.

Pia wamesema kuwa kauli za serikali kuwa kuna makundi yasiyoitakiwa nchi amani, si za kweli, bali makundi yaliyopo yanasababishwa na kutokuwepo uwiano mzuri wa maisha au mali, kati ya viongozi na wananchi, haki kupotea kwa wanyonge na hali ya maisha kubadilika kila wakati huku wengine wakiishi 'kama wako Ulaya'. 

Hayo yalisemwa juzi katika Chuo cha Kanisa la Pentekosti la Yombo Matangini, Dar es Salaam wakati wa mahafali ya sita ya Walimu 18 Maalumu wa kutoa mafunzo kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano juu ya ukristo, ikiwa ni mikakati ya kuandaa kizazi cha kujua madhehebu hayo.

Walisema kuna haja kubwa ya viongozi wa serikali kusikiliza hotuba za Hayati Mwalimu Julius Nyerere na matazamo wake ili kutumia mfumo huo kuongezea nchi, huku wakifafanua kuwa tangu afariki hajapatikana kiongozi mwenye dhamira kama yake.

"Watanzania ni watulivu na wanapenda haki lakini serikali imeshindwa kutambua haki ndio msingi wa taifa na badala yake imekuwa ikishikana mashati na vyama vya siasa na kulaumu baadhi ya viongozi wa dini," alisema Bw. Erick Mwasyoge ambaye pia ni mchungaji na mkuu wa chuo cha kanisa hilo.

Alisema cha kushangaza Tanzania ni ya tatu duniani kuwa na rasilimali nyingi pia ni ya tatu kwa umaskini baada ya kushindwa kuzitumia na kuwaachia watu wa nje kuzimiliki.

Maaskofu waliohudhuria katika mahafali hayo ni wawili kutoka Mbagala na Ukonga, wachungaji 14 na mwinjilisti mmoja ambao kila mmoja alipewa nafasi ya kuzungumza juu ya hali halisi ya ukristo nchini.

Wachungaji hao waliweka hadharani mapungufu ya madhehebu yao na kuonesha wasiwasi kuwa dunia itatekwa na dini ya kiislamu kwa kile walichodai ni ujenzi imara wa misingi katika kizazi chao cha sasa, huku wakristo waking'anga'ania madaraka na utajiri.

Hata hivyo, Askofu wa Kanisa la Salvation and Healing Pentecoste lililopo Mbagala Kibondemaji, Bw. Isack Mchome alisema kuwa watoto wameharibika  kutokana na kukosa maadili ya wazazi ambapo hivi sasa wanaishi kulingana na wanachokiona kwenye mitandao ya sayansi na teknolojia.

Alisema mtu wa kwanza anayetegemewa na taifa kutoa maadili ni viongozi wa dini na kwamba kinachohubiriwa ndani ya kanisa ni juu ya kupata mali na kutoa ushuhuda huku wakishindwa kuhubiri neno la Mungu.

"Nyumba nzuri ni ile iliyowekewa msingi imara hivyo tusipoandaa kizazi chenye maadili ya ukristo ambacho kitarithi basi tutakwama, isitoshe mfumo huu wa ukristo wa kung'ang'ania maadilizi ya leo ya watu wakubwa,  kesho hautakuwa na matunda mazuri," alisema.

1 comment:

  1. MWENYE MACHO HAAMBIWI TIZAMA SIKILIZA MANENO YA WACHUNGAJI KUHUSU MAPUNGUFU YA MADHEHEBU YAO.TUNAWAPONGEZA KWA KULIJUWA HILO NI VEMA UKATOA KIBANZI KILICHO JICHONI
    MWAKO HALAFU UMWELEKEZEE MWENZIO

    ReplyDelete