10 May 2011

Shirikisho la kisiasa EAC bado moto

Na Gladness Mboma

BARAZA la Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki limeiagiza timu ya watalaamu iandae mapendekezo thabiti yatakayowezesha kukabiliana na hofu, kero na
changamoto za kuanzisha shirikisho la kisiasa zilizoainishwa na Wanaafrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhusu mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri na Mkutano wa tisa wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mapendekezo hayo ya watalaamu yatatakiwa kuwasilishwa katika mkutano wa 13 wa wakuu wa nchi unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

"Wakuu wa nchi walipokea taarifa ya mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusiana na timu ya Wataalamu iliyoundwa kuainisha hofu, kero na changamoto za kuanzisha shirikisho la kisiasa zilizoainishwa na Wanaafrika Mashariki na kutoa mapendekezo ya kupambana nazo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika mkutano huo wakuu wa nchi walimteua Balozi Dkt. Richard Sezibera kutoka Jamhuri ya Rwanda kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya kujaza nafasi ya Balozi Juma Mwapachu aliyemaliza muda wake.

Pia Wakuu wa Nchi walimteua Dkt. Enos Bukuku kutoka Tanzania kuwa Naibu Katibu Mkuu atakayesimamia sekta ya mipango na miundombinu, uteuzi ambao ulianza rasmi Aprili 25, mwaka huu, ambapo pia Jaji Isaac Leonala kutoka Jamhuri ya Kenya aliteuliwa Jaji katika mahakama ya Sheria ya Jumuiya kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wakuu hao wa nchi walipokea taarifa kutoka Baraza la Mawaziri kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Umoja wa Forodha na Mapendekezo ya kuanzishwa eneo moja la Forodha.

Wakuu hao wa nchi walikubaliana na mapendekezo ya baraza hilo na kuagiza sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uchambuzi wa kina kuainisha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa umoja wa forodha na kubainisha upungufu wa kutoa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji wa maeneo yaliyosalia ili kufikia umoja wa forodha kamili.

Pia Baraza la Mawaziri lilipokea taarifa ya mpango wa uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs) na kuzitaka nchi wanachama kuchukua hatua za haraka ili kuondoa vikwazo hivyo, kutoanzisha vipya na kuagiza sekretarieti ya Jumuiya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji kwenye mkutano ujao wa Baraza la kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji.

No comments:

Post a Comment