11 May 2011

Kili Taifa Cup yapigiwa debe

Na Daud Magesa, Mwanza

MICHUANO ya Kili Taifa Cup, imepigiwa debe kuwa ni chachu ya maendeleo ya soka nchini katika kuibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi kwa manufaa ya
taifa.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MRFA), Jackson Songora wakati akikabidhi vifaa kwa timu za kituo cha Mwanza zinazoshriki michuano ya mwaka huu kutoka Kanda ya Ziwa.

Alisema Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo ndiyo mdhamini Mkuu wa michuano hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro, haina budi kupongezwa kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza  soka nchini hapa.

Mwenyekiti huyo alisema TBL inapaswa kuungwa mkono na wadau kuhakikisha michuano ya Kili Taifa Cup inafanyika kwa mafanikio makubwa.

Michuano hiyo ya Taifa, msimu huu ilianza Mei saba mwaka huu katika vituo sita kwa timu za mikoa mbalimbali kujitupa kuwania ubingwa huo wa taifa.

Songora alisema mashindano hiyo ni muhimu kutokana na kuibua vipaji vingi vya soka vinavyotamba hapa nchini.

Kwa mujibu wa ratiba, michezo hiyo ya makundi inamalizika leo katika vituo vyote ambapo katika kituo cha Mwanza, wenyeji  'Mwanza Heroes' watahitimisha kwa kuumana na Mara Stars saa 9 alasiri, wakati Shinyanga 'Igembesabho' wao watamaliza na Kagera 'Lweru Eagles' saa 8:00 mchana.

No comments:

Post a Comment