30 May 2011

Mwambusi ataja siri ya ubingwa Kili Cup

Na Mwandishi Wetu, Arusha

BAADA ya kutwaa ubingwa wa Taifa 'Kili Taifa Cup 2011', kocha wa timu ya Mkoa wa Mbeya 'Mapinduzi Stars', Juma Mwambusi amesema siri ya ushindi wa
timu yake ni ushirikiano uliokuwepo.

Akizugumza mjini hapa juzi, wakati wa chakula cha usiku kilichoandaliwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro kwa ajili ya kuzipongeza timu zilizochukua nafasi tatu za juu, Mwambusi alisema kikosi chake kilikuwa kina  ushirikiano mkubwa tangu hatua ya makundi.

Alisema kikosi chake tangu kilipoanza mashindano hayo kilikuwa kikijituma na kila mchezaji akitoa nafasi kwa mwenzake, hivyo kuwapa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa huo.

"Siri kubwa ni ushirikiano wa wachezaji wakiwa uwanjani, viongozi na hata benchi la ufundi nina amini kila kitu kinawezekana nawapongeza sana," alisema Mwambusi.

Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mwanza ambayo imeshika nafasi ya pili John Tegete, alisema timu yake kufikia hatua ya fainali si kazi rahisi hivyo aliipongeza timu hiyo hasa ikizingatiwa haikufanya vizuri katika mashindano ya mwaka jana.

Alisema matarajio yake yalikuwa kombe hilo liende mwanza, lakini bahati haikuwa yao timu yao imeshika nafasi ya pili na kuondoka na kitita cha sh. milioni 20.

Tegete alisema mashindano yalikuwa mazuri kwa kuwa kila timu ilionesha upinzani mkali lakini timu yao ikafika hatua ngumu ya fainali ambayo kila mtu alikuwa akiitaka.

Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Athuman Nyamlani, aliwapongeza viongozi wa chama cha Mpira wa Miguu Mkoa Arusha (ARFA) kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kipindi cha mashindano.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe naye aliipongeza TFF kwa kuendesha mashindano vizuri ambayo yalileta msisimko mkubwa katika Mkoa wa Arusha.

“Mashinado yamekuwa mazuri na naishukuru TFF, waandishi wa habari na wadau wote waliofanikisha mashindano ya mwaka huu,” alisema Kavishe.

No comments:

Post a Comment