Amina Athumani
MKUFUNZI wa kimataifa wa mpira wa kikapu kutoka Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo (FIBA), Vitali Gode jana amefungua kozi kwa waamuzi wa kwa ajili ya
kuwanoa ili wafikie kiwango cha kuchezesha nchi za Kanda ya tano.
Kozi hiyo ambayo inashirikisha Watanzania pekee imefunguliwa katika Ukumbi wa Don Bosco, Dar es Salaam ambapo jumla ya waamuzi 10 wamejitokeza kushiriki kozi hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kozi hiyo, Gode alisema mwamko wa waamuzi kujitokeza kushiriki kozi hiyo umekuwa ni mdogo na alitegemea angekutana na waamuzi wengi kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
"Waamuzi ni sehemu muhimu katika michezo kwa kuwa bila waamuzi hakuna mchezo huru utakaotoa mshindi halali, hivyo natoa wito kwa Watanzania na waamuzi ambao wapo kwenye mikoa mingine nje ya Dar es Salaam wanapoona fursa kama hii inajitokeza, basi waichangamkie," alisema Gode.
Naye Katibu Msaidizi wa TBF, Michael Maluwe alisema kozi hiyo yenye kiwango cha cha kimataifa, itaendeshwa kwa siku nne na itaendeshwa na FIBA Afrika kwa kushirikiana na TBF.
Alisema waamuzi watakaofaulu katika kozi hiyo watapangiwa na FIBA, kusimamia mashindano ya kanda ya tano yatakayofanyika jijini Dar es Salaam Agosti mwaka huu.
Waamuzi wanaoshiriki mafunzo hayo ni Magana Onaventura, Haleluya Kavarambi, Said Hamisi, Amani Kitumari, Baraka Rashid, Jaqueline Shemeza, Kaisua Kiwele, Hadija Karambo na Diana Deodatus.
No comments:
Post a Comment