Na Shufaa Lyimo
TIMU Ya Moro United Tabata, Dar es Salaam inasaka wachezaji vijana wenye umri chini ya miaka 20, kupitia mashindano ya Street Cup ambayo yafanyika kila
wikiendi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Tabata.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa timu hiyo, Rojaz Peter alisema lengo la kusaka vijana hao ni kuongeza nguvu kwenye timu yao ya vijana, ambao kati yao watawasajili msimu ujayo kuichezea timu kubwa.
Alisema ameamua kufuatilia mashindano hayo, baada ya kugundua mitaani kuna vijana wengi wazuri wenye vipaji vya soka, isipokuwa wanashindwa kuvitumia kutokana na kukosa walezi.
"Mashindano haya yanaibua vipaji vingi ndiyo maana tunayafuatilia kwa kina kwa sababu sisi ni watu wa Tabata, hivyo lazima tuchukue wachezaji waili au watatu kutoka hapa ndipo tuweze kutoka nje," alisema Mwenyekiti huyo.
Peter alisema pindi Ligi Kuu ya msimu ujao itakapoanza watakuwa tayari wamepata wachezaji wanaowahitaji katika timu B, ambao watawanoa na kusajili katika msimu ujao.
"Mpaka Ligi Kuu itakapoanza tena tayari tutakuwa tumepata vijana tunaowahitaji kwa sababu hatutaki kuwa na wachezaji ambao viwango vyao vipo chini, bali tunataka watakaoleta ushindani kwenye timu," alisema.
Wakati huo huo Peter alisema msimu ujao wa Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu wataingia uwanjani na staili mpya kwa lengo la kujikinga ili waishuke daraja kirahisi kama ilivyokuwa misimu ya nyuma.
No comments:
Post a Comment