Na Addolph Bruno
MHAMBULIAJI wa timu ya taifa 'Taifa Stars' Athumani Machupa, anayecheza soka la kulipwa nchini Sweden ametua nchini juzi usiku kuiongezea nguvu Stars
kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya Afrika ya Kati zitakazofanyika mwakani katika nchi za Gabon na Guinea ya Ikweta.
Mbali na Machupa mchezaji mwingine aliyewasili ni mshambuliaji, Mbwana Samatha aliyetua nchini juzi akitokea Jamhuri ya kidemkrasi ya Congo (DRC), katika klabu yake ya TP Mazembe kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa Juni 5 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema wachezaji hao walitarajiwa kujiunga na wenzao kufanya mazoezi jana jioni katika Uwanja wa Karume, Jijini.
Alisema mbali na wachezaji waliowasili wengine, Abdi Kassim 'Babi' na Danny Mrwanda wanaochezea Klabu ya DT Dong Long ya nchini Vietnam watawasili nchini leo saa 7 mchana.
Wambura alisema kwa upande wa kiungo Idrisa Rajabu, anayekipiga katika Klabu ya SofaPaka ya Kenya alitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo akitokea Tunisia ambako timu yake ilikuwa inacheza michuano ya Shirikisho.
"Kwa ujumla maandalizi yanaendelea vizuri, uhakika wa wachezaji wa nje kuja ni mkubwa na timu itarajia kuondoka nchini Juni 3 asubuhi kwenda Afrika ya Kati kwa ajili ya mechi hiyo," alisema Wambura.
Wambura alisema mshambuliaji, Nizar Khalfan atakuwa mchezaji wa mwisho kuwasili nchini kwa ajili ya maandalizi, kabla ya mechi Juni Mosi mwaka huu akitokea Canada anakocheza katika Klabu ya Vancouver White Caps.
No comments:
Post a Comment