Na Tumaini Makene
WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo kikimalizia ngwe ya Operesheni Sangara kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kufanya maandamano
Iringa Mjini, kimesema kuwa kitahakikisha kuwa miaka mitano ya awamu ya mwisho ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete itakuwa ya mchakamchaka, kuwajibika kwa wananchi na kuondoa umaskini.
CHADEMA kimesema kuwa hawatakubali Rais Kikwete alale ilihali maisha ya Watazania wengi wanyonge yakingali ya kubahatisha, wakiwa hawana uhakika wa maisha bora kwa kupata huduma za jamii zinazowastahili kama vile elimu, afya, kutengeneza fursa za wao kujipatia kipato, ikiwa ni moja ya nyenzo muhimu katika kupambana na umaskini.
Akizungumza katika mikutano yake mitatu kwa siku ya jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, alisema kuwa kitaendelea kusimama kidete upande wa wananchi, kuhakikisha wananchi wanapata haki stahili kutoka kwa serikali yao,kadri ilivyoahidi na kupewa dhamana ya kuongoza nchi.
Akiwahutubia wakazi wa Ilula, Bw. Mbowe alisema "CCM leo ni kama wamechanganyikiwa, hawana tena mbinu wala mikakati ya kuisaidia nchi hii na wananchi wake. Umaskini unazidi kuongezeka, ukali wa maisha unawamaliza Watanzania, gharama za maisha zimepaa...lakini Watanzania wengi hawajui uhusiano wa umaskini wao na utawala mbovu wa serikali ya CCM.
"Wengine ukiwauliza hawajui hata kama wanalipa kodi...wanajua kodi ilishafutwa, kodi ya kichwa, kodi ya manyanyaso...wakipata huduma kidogo kutoka serikalini wanafikiri ni zawadi, wanafikiri serikali imewafanyia hisani...ndiyo maana tunakuja huku kuwaamusha na kuwaelimisha Watanzania, juu ya kutimiza wajibu wao na kudai haki zao.
"Wananchi tunasema tutahakikisha serikali hii hailali tena, tunamwambia Kikwete ikulu itakuwa chungu, serikali lazima iwajibike kwa wananchi wake, wananchi wanahitaji kuona serikali ikiwajibika...Rais Kikwete tutakufanya ufanye kazi usiku na mchana...sijui mnajivua gamba, sijui semina elekezi, sijui kitu gani, hatujui, lakini wananchi wanahitaji maisha bora," alisema Bw. Mbowe.
Alisema si sahihi kwa taifa lenye utajiri wa rasilimali za kila aina, wananchi wake kuendelea kuogelea katika umaskini mkubwa, ambao sasa umekolezwa makali na kupanda kwa gharama za maisha, huku hali ya kipato ikibaki kuwa ile ile au kushuka, huku maskini hao hao wakilipishwa kodi kila kukicha kupitia bidhaa na huduma mbalimbali.
Alisema kuwa sasa ni wakati mwafaka kwa Watanzania kunufaika na rasilimali zao, huku akiitaka serikali kupanua wigo wa utozaji kodi, kuwatoza wawekezaji wakubwa, badala ya kuendelea kuwakandamiza wananchi maskini katika kila mwaka wa bajeti kwa kuongeza kodi katika bidhaa na huduma wanazotumia karibu kila siku.
Akiwa kijijini Ifunda Bw. Mbowe aliombwa kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa mwaka jana wakati wa uchaguzi, mojawapo ikiwa ni ahadi ya mgombea urais kupitia CCM, Rais Kikwete juu ya kumaliza kero ya maji maeneo hayo.
Wakazi hao walilalamika kutotekelezwa kwa ahadi ya maji iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete mwaka jana wakati wa kampeni za kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu, ambapo walisema kuwa aliahidi kutoa takribani sh. milioni 600 ili kumaliza tatizo la uhaba wa maji kijijini hapo.
Mkazi mwingine aitwaye Hidaya Mwagao, alilalamika jinsi alivyolazimika kujifungua katika zahanati ya kijijini hapo usiku, ambapo wakunga walilazimika kutumia simu za tochi kumulika wakati wa kumhudumia, ilihali zahanati hiyo iko hatua chache kutoka mahali lilipo soko ambalo lina umeme.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Grace Kiwelu alisema kuwa ni aibu kwa wananchi katika taifa lenye umri wa miaka 50 likiwa na rasilimali za kila aina kuendelea kuwa kero ya maji safi, huku viongozi wao wakionekana kutokujali.
Taifa hili ni kubwa, kama ahadi ilitolewa na mh. Raisi je viongozi waliopo huko walichukua hatua gani?Raisi hana tatizo ila wasaidizi wake
ReplyDeletendugu hapo juu unakosea, Kosa ni la Rais kwanini hawachukulii hatua wahusika wake aliowateua wasiowajibika. kazi ya rais siyo kuifanya kazi husika lakini yeye ni msimamizi mkuu kuakikisha ahadi zake zimetekelezwa. Taifa kubwa siyo hoja kwani unawawakilishi kila kona ya Tanzania kwahiyo unaweza kupata taarifa yeyote unayoitaka na ndio maana tunakupa nyenzo zote ikiwemo wasaidizi kibao wakukusaidia na kama hawafanyi kazi inavyotakiwa watimue ajiri wengine kwani kazi ya rais si kuteua watu tu bali pia kuwatimua wale ambao hawatekelezi wajibu wao.
ReplyDeleteKama ukubwa wa nchi ni Leo Ndio mnajua? Ndio maana alipoulizwa rais wake kwanini nchi hii ni masikini kuliko na rasilimali, Amani nk akasema hajui. No hope here!
ReplyDelete