19 May 2011

Waliokufa ajali Geita watambuliwa

Na Faida Muyomba, Geita

WAKATI miili ya watu wanane waliokufa katika ajali wilaya Geita mkoani mwanza juzi wametambulia, Dereva wa basi la Bunda lililogongana na jingine la Sheraton na
kusababisha ajali hiyo amekamatwa.

Katika ajali hiyo watu 16 walikufa na wengine 58 kujeruhiwa ika kijiji cha Chibingo wilayani humo.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Bw. Nonosius Komba alimtaja dereva ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo kutokea kuwa ni Bw. Karamdin Hussein(45) mkazi wa jijini Mwanza.

Alisema kuwa bado wanamtafuta dereva mwenzake wa basi la Sheraton, Bw. Enos ambaye naye alitoweka na wamemwamuru mmliki wa basi hilo kuhakikisha anampata ambapo alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani wakati wowote.

Aliitaja miili ya watu waliotambuliwa kuwa ni wa Askari Polisi G.3642 PC Peter Onesmo Mashala ambaye alikuwa akifanya kazi Kituo Kikuu Mwanza.

Wengine ni Bw. Maneno Ngasa (27) mkazi wa Sengerema, Bw. Hassan (30) mkazi wa Bukoba, Bw. Samson Senga (30) na Masumbuko Paul (5) mkazi wa Bukoba

Wengine ni Bw. Deogratius Makungu (40) mkazi wa Geita, Bw. Johnson Nyoni(45), Bw. Daniel Zablon (26) mkazi wa Nyakato na wote wamechukuliwa na ndugu zao.

Kamanda Komba alisema, miili ya maiti wengine bado haijatambuliwa na jeshi hilo limetoa fursa kwa watu mbalimbali kufika Hospitali ya Wilaya ya Geita kuwatambua ndugu zao huku akiushukuru Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa msaada wa magari pamoja na dawa kwa ajili ya majeruhi.

Katika hatua nyingine majeruhi 23 kati ya 58 waliokuwa wamelazwa kutokana na ajali hiyo wameruhusiwa kuondoka baada ya hali zao kuimarika.Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo, aliiambia Majira kuwa majeruhi hao waliruhusiwa jana asubuhi na kwamba wamebaki 35 wakiendelea na matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hamis Kagasheki alisema serikali imesikitishwa sana na vifo hivyo, hivyo akawataka madereva kuwa kufuata sheria za barabarani ili kunusuru maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

1 comment:

  1. HIVI AJALI KILA SIKU TANZANIA HAKUNA VIONGOZI WANAFUATILIA VIFO VYA KILA SIKU VYA AJALI?
    IKIWA nchi kama Uingereza magari yapo mengi lakini ajali ni chache sana inamaanisha TANZANIA INA MAGARI MENGI ndio maana ajali ni nyingi jamani,tufike mwisho sisi Watanzania tukatae ajli kwa kuwaambia viongozi wetu kufuatilia utendaji sio kukopi taarifa za miaka ya nyuma

    ReplyDelete