10 May 2011

Kikwete abaini kutoelewana serikalini

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa ipo kasoro kubwa baina ya watendaji wakuu serikalini, Makatibu Wakuu na Mawaziri ambao wamekuwa na mahusiano mabaya na
viongozi wenzao wa chini jambo ambalo alisema kuwa ni hatari kwa serikali.

Kutokana na hali hiyo Rais Kikwete alisema kuwa wizara haziendeshwi kama idara ya usalama, na uongozi siyo mbio za riadha kuwa kiongozi lazima ashirikiane na wenzake katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali ndani ya wizara husika.

Alisema kuwa viongozi lazima washirikiane, wakutane na wajengeane staha, kwani imefika wakati hivi sasa kuna watendaji ambao wamekuwa wakipingana hadharani na kuchukuliwa kwenye vyombo vya habari, hali ambayo alisema kuwa si maadili mema ya kazi.

Alisema kuwa hilo limejidhihirisha pale inapoonekana kuna miingiliano ya maamuzi, kwani wapo watendaji ambao hawapendi wenzao wasikike, suala ambalo alisema kuwa si sahihi kwani ndani ya wizara ni vema watu wapeane majukumu na si mmojawapo kukumbatia kila kitu.

Alionya kuwa pale mtu atakapoona vigumu kugawa madaraka kwa wengine na kama haafiki hivyo ni bora atoke.

Kikwete aliyasema hayo jana wakati akifungua semina ya mafunzo elekezi kwa viongozi na watendaji wakuu wa serikali iliyofanyika mjini Dodoma.

Alisema kuwa baadhi ya makatibu wakuu kutokuwa na mahusiano mazuri na manaibu makatibu wakuu; na hata mawaziri nao kutokuwa na mahusiano mazuri na manaibu wao kumekuwa kukisababisha wengine kukosa kazi za kufanya katika maeneo hayo hali ambayo alisema kuwa ni fedheha kwa nchi.

Rais Kikwete aliwatisha viongozi hao: “Kwa kweli nashangaa imefika wakati viongozi mnachimbana wenyewe kwa wenyewe wakati aliyewateua na kuwaweka hapo mlipo haoni sababu ya kuwachimba, na ndiye mwenye mamlaka ya kukuweka na kukutoa tena ukajisikia tu kwenye vyombo vya habari kuwa nafasi ulikuwa nayo sasa haupo nayo,” alisema.

Alisema kuwa wakati wa uteuzi wake kwa viongozi hao aliwakabidhi Ilani ya utekelezaji wa mambo mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano na hiyo ndiyo dira ya mwongozo wa utendaji kazi kwa viongozi hao na kila kiongozi anapaswa kuandaa mpango kazi wake.

Rais alisema kuwa viongozi hao hawapaswi kuwa wavivu na wasiopenda  kusoma vizuri ilani hiyo na kuielewa kwa wao ni viongozi wa kuwasidia wananchi katika kuwaletea maendeleo, si wa kukaa maofisini na kusoma magazeti.

Alisema kuwa yeye si rais aliyeteua viongozi wa kusoma magazeti ofisini, kuangalia TV na kunywa chai na hata kusoma mafaili, bali aliteua viongozi ambao watakuwa karibu na wananchi katika kuwatatulia kero zao mbalimbali ikiwemo elimu, maji, barabara, afya lakini hilo halifanyiki inavyotakiwa.

Kutokana na hali hiyo rais alitoa agizo la viongozi hao kutoka na kwenda kwa wananchi na kujua mambo yanayowasumbua kwani hakuna wizara ambayo aliiteua kazi zake zikawa ni za ofisini na haziwahusu wananchi.

Alisema kuwa kwa muda wa kipindi cha miezi sita tangu amewateua viongozi hao hawasikii katika vyombo vya habari wakishirikiana na wananchi katika kuwatatulia kero zao na kusema kuwa viongozi hao wamekuwa na kazi gani kubwa ambayo imekuwa ikiwafanya washindwe kuwa karibu na wananchi ambao wamewapa dhamana ya kuwepo madarakani.

Hata hivyo, alisema kuwa suala la kwenda kwa wananchi si la mawaziri peke yao hata makatibu wakuu nao wanapaswa kufanya hivyo kwani wao ndiyo mhimu sana na ndiyo waidhinishaji wa fedha nyingi za miradi ya maendeleo hivyo wanapaswa kwenda vijijini ili kuona kama utekelezaji wa fedha wanazoidhinisha zinatumika kama ilivyokusudiwa kwani kila mmoja wao yupo  katika shughuli ambazo zipo chini ya jamii.

Vile vile alisema kuwa mawaziri wasiwe wa kushughulikia madokezo wakiwa maofisini tu kwani kufanya hivyo ni kupoteza fedha za umma kwani uvivu wa kutembelea miradi inayotekelezwa ni hatari, kwani wanaweza kudanganywa na watekelezaji wa chini kwa kigezo cha kutumia uvivu wao.

Aliwataka viongozi kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kuwaparanganyisha kwa kuwa uongozi si mashindano ya riadha, kwamba kiongozi ni mtu mmoja peke yake,  hivyo ndani ya wizara mtu asitegemee kuwa anawaweza kuongoza wizara peke yake, hivyo lazima wakumbuke dhana ya uwajibikaji wa pamoja.

Vile vile alitoa angalizo kwa miswada mbalimbali ya serikali  inayowasilishwa bungeni, kuwa mawaziri wanapaswa kuwa wamoja pale muswada wa serikali unapowasilishwa na kuunga mkono na kuupitisha, na hatarajii kuona waziri kupingana na mwingine kuupinga muswada, kwani kufanya hivyo ni kukiuka misingi ya utawala bora na kanuni haziruhusu.

Ingawa hakutaja jina, katika Mkutano wa Bunge uliopita, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alitofautiana na mawaziri na wabunge wa CCM pale alipokubaliana na mapendekekezo ya Msemaji wa Upinzani katika kupitisha vifungu vya mudwada wa Sheria ya Mahakama.

Rais Kikwete pia alikemea uzembe, wizi, mipango ya kuchonga laini za fedha, ubadhilifu, utovu wa nidhamu, uzizi, majigambo, dhuluma, akisema mambo hayo si sifa nzuri kwa makatibu wakuu, mawaziri na hata manaibu kwani wao ni viongozi wakubwa serikalini.

Awali, akimkaribisha Rais Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo alisema kuwa mafunzo hayo ya semina elekezi kwa watendaji wa serikali  yatahusu mambo mbalimbali ya kiutawala, uchumi na maendeleo, utawala bora pamoja na masuala mengineyo na yale ya mtambuka ambapo watoa mada ni kutoka Benki ya Dunia, Jamhuri ya Afrika Kusini na wengine ni Watanzania waliowahi kutumikia serikalini na wengine wakiwa bado serikalini.

Semina hiyo imegharamiwa na serikali pamoja na taasisi mbalimbali  wakiwemo Bima ya Afya, Mamlaka ya Udhibiti wa Bima, Sumatra, CRDB, Tanapa, TRA na NMB.

5 comments:

  1. Du! Hii SeriKali kwa Semina Elekezi Tu Inaongoza

    ReplyDelete
  2. Kwao wakishajikusanyia kodi kidogo tu badala ya kujenga madarasa na madaraja,wnaziwekea kikao cha kuzitafuna,tutafika?? lakini Mungu Atusamehe kwani tulijichagulia wenyewe viongozi hawa.Tuvumilia labda 2015,Mungu atatusamehe tukimtii.

    ReplyDelete
  3. Kutofautiana bwana JK ni suala la kawaida kabisa. Wengine ulowaweka katika baraza lako la mawaziri siyo vilaza na wasanii kama wewe mwenyewe na ndo maana wanaku-against na mambo mengi ndani ya serikali yako. It's shame Mr. President on what is happening now, na hii ina-prove failure ya utawala wako. UMESHINDWA WEWE, CAN'T YOU JUST STEP ASIDE!

    ReplyDelete
  4. Wao ni vikao, semina, warsha, mikutano, yote walipane posho tu!
    Ukiuliza kwanini wasiende moja kwa moja kwa wananchi ili wajue matatizo yao, watasema wako "busy"!
    CCM na vibaraka wao hawawezi na hawataweza kutukomboa na kuutokomeza umaskini na kutuletea maendeleo.
    Wao ni ufisadi, wizi, uvivu, kujilimbikizia mali, rushwa na ubadhirifu.
    Bure kabisa!

    ReplyDelete
  5. Yaani Rais mzima unasema mawaziri wasipinge muswada kwa sababu unatoka CCM sasa kama una itilafu waukubali tu? na kama utatumia kodi ya mlalahoi bila kuleta maendeleo? That's must be the dumbest thing President can say....

    ReplyDelete