10 May 2011

Serikali haijashindwa kulipa mishahara-Mkulo

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

SERIKALI imekanusha madai ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe kuwa imeshindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake posho na mishahara ya wabunge, huku
ikisema fedha zipo za kutosha na hata ziada, hivyo madai ya mbunge huyo ni uongo wa kujitafutia umaarufu.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Fedha, Mustapha Mkullo na kusema kuwa serikali inawalipa watumishi wake mishahara yake kama kwaida kwa kutumia mapato yake ya ndani kwani serikali bado inaouwezo hata wa  kugharamia shughuli zake nyingine, pamoja na gharama za kuendesha bunge.

“Napenda kutumia fursa hii kukanusha vikali madai ya uongo na upotoshaji uliofanywa kwa maksudi kwa lengo la mtu kujitafutia umaarufu wa kisiasa na natumia fursa hii kuwaeleza kuwa taarifa hizi sio sahihi," alisema Bw. Mkulo.

Bw. Mkulo alitoa taarifa hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kunukuliwa na  gazeti moja la kila siku akisema hawezi kujibu habari za barabarani za CHADEMA.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Ramadhan Kijjah, alikaririwa na gazeti jingine jana akikiri kuchelewa kwa mishahara ya wabunge, lakini akasema tatizo ni la hazina na Kamishana wa bajeti, ambao wangeweza kueleza sababu za kuchelewa huko.

Hata hivyo katika kuweka mambo sawa, Waziri Mkulo alilazimika kueleza umma kuwa Desemba mwaka jana mapato yaliyokuswanywa yalikuwa sh. bilioni 594 wakati mishahara ililipwa sh. bilioni 243.8 na kubaki ziada ya sh. bilioni 350.20

Alifafanua kuwa January mwaka huu selikali likusanya sh. bilioni 433.5 wakati ililipa mshahara sh. bilioni 240 na kubaki na ziada ya sh. bilioni 193.50 wakati Februari walikusanya sh. bilioni 430.40 wakalipa mishahara sh. bilioni 266.70 na kubaki na ziada ya sh. bilioni 163.70.

Lakini Bw. Mkulo alisema kuwa Machi mwaka huu, serikali ilikusanya sh. bilioni 567 na kulipa mishahara sh. bilioni 249.5 na kubaki na ziada ya sh. bilioni 317.60 na Aprili walikusanya bilioni 432 wakalipa mshahara sh. bilioni 246.70 na kubaki na ziada ya bilioni 185.40.

"Kwa kawaida serikali inatumia fedha taslimu kulipa gharama zake, kwa hiyo mapato ya Desemba yanalipa mishahara na matumizi mengine ya Januari mapato ya Januari yanalipa matumizi ya Februari na kadhalika. Kwa utaratibu huu hakuna hata mwezi mmoja ambao wafanyakazi wa serikali wamekosa mshahara,” alisema.

Aidha, alisema serikali haijashindwa kugharamia posho mbalimbali za wabunge pamoja kuwa gharama hizo zilizidi kutokana na kufanyika kwa semina elekezi kwa wabunge kuhusu kanuni mbalimbali za bunge kutokana na kuwepo kwa asilimia kubwa ya wabunge wapya.

Alisema kuwa mwezi uliopita fedha za mishahara ya wabunge zilitolewa Aprili 22 na fedha kwa ajili ya posho nazo zilishatolewa kwenye ofisi ya bunge, huyo mbunge aliyetoa madai hayo na yeye ameshapata," alisema Mkullo.

Waziri huyo alibainisha kuwa pamoja na kutumia mapato ya ndani katika shughuli zake, serikali hukopa kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kugharamia shughuli za maendeleo.

Akizungumzia suala la mikopo kutoka katika vyanzo mbalimbai alisema mikopo hiyo hutumika kugharamia shughuli za maendeleo na hasa za uendelezaji wa miundombinu.

Alisema kuwa kwa mwaka 2010/11 serikali ilipanga kukopa kiasi cha dola za Marekani milioni 525 kati ya kiasi hicho dola milioni 250 zitatumika kugharamia miundombinu ya barabara na dola milioni 175 zitatumika kwa ajili ya kununulia mitambo ya kufua umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 kwa Jiji la Dar es Saalam na megawati 60 kwa ajili ya Mwanza.

Waziri huyo aliwataka wananchi kupuuza madai ya Bw. Kabwe ambayo aliyatoa mkoani Mbeya na kusema kuwa mbunge huyo ameanza kusema uongo usiokuwa na msingi na kuwapotosha wananchi kuwa serikali yao imefirisika kitu ambacho si cha kweli.

Akizungumzia hatua zitakazoendelea dhidi ya mbunge huyo, Bw. Mkulo alisema kuwa ni kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kazi ambayo ni ya Spika na Katibu wa Bunge.

1 comment:

  1. Mh. Mkulo inakuwa ngumu sana kwa sisi wananchi kukuamini, maana mambo yanavyokwenda tunaona siyo kabisa. Unavyoeleza ni kisiasa zaidi na si kiutekelezaji/hali halisi. AAu ufanisi wa serikali yetu upo ngazi za juu tu. Mfano sisi wanafunzi tulio nje ya nchi ambao serikali ya Tanzania inabidi ichangie gharama, mara nyingi hatulipwi kwa wakati. Na kwa mwezi huu wa tano hadi leo tar 10 hatujapata pesa ya kujikimu, je kutokana na hili tutaacha kumuamini Mh. Zitto? Tumekuwa tunataabika sana nchi za watu na kufikia kuathiri ufanisi wetu. Tumeshapoteza uaminifu na wanaosimamia pango la vyumba vyetu, hatuwezi kusafiri kwa public transport (inabidi tutembee umbali mrefu) na kula yetu ni ya taabu mno sasa. Tumeshalalamika sana mpaka tumekata tamaa.

    ReplyDelete