11 May 2011

Fergie awapangia mikakati Iniesta, Xavi, Messi

LONDON, Uingereza

ALEX Ferguson jana usiku ameeleza kuhusu mikakati yake ya kuidhibiti Barcelona, katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayochezwa Mei 28, mwaka huu kwenye
Uwanja wa Wembley.

Kocha huyo anayepigania historia ya kuipatia ubingwa wa Ulaya, Manchester United kwa mara ya tatu alisema moja kati ya mbinu atakayoitumia ni kushambulia kwa muda wote.

Bosi huyo wa United ametoa kauli hiyo baada ya siku kadhaa za kusikia wapinzani wake wakipongezwa na kupewa nafasi zaidi ikilinganishwa na timu yake.

Fergie alisema: "Tuna wachezaji ambao wanaweza kuifanya timu yoyote kuwa na usumbufu mkubwa.

"Ninatumaini washambuliaji wote waletea matatizo, ambao watu wanafikiri kuwa watatuletea sisi.

"Kila mmoja anajua ni kwa jinsi gani timu ya Barcelona ilivyo kubwa lakini, Manchester United iko katika fainali.

"Kila mmoja anasema kuwa Manchester United si timu nzuri, hatuko hivi au vile. Lakini timu yetu imefunga magoli mengi kuliko yoyote ile. Kiwango chetu nyumbani kimekuwa cha kusisimua. Hatujafungwa katika mashindano ya Ulaya.

"Tuko katika fainali ya Ligi ya Mabingwa na tutatwaa ubingwa wa Ligi kwa kupata pointi moja zaidi.

"Ninatakiwa kuwa mkweli wakati ninapoingalia timu yangu na kujiuliza 'nimeridhika?' Wachezaji wamenipatia mimi kila kitu."

Ferguson anafurahia kupata mechi ya kulipa kisasi baada ya kufungwa na Barca, katika fainali ya mwaka 2009 na anajua kuwa ni lazima vijana wake kuwadhibitia Xavi, Andres Iniesta na Lionel Messi.

Kocha huyo alisema: "Katika fainali mara ya mwisho hatukuanza vizuri, kisha kutoa goli.
"Tunachotakiwa kufanya ni kutafuta dawa ya matatizo ya Xavi, Messi na Iniesta.

"Kila mmoja amekuwa akisaka dawa hiyo kwa sababu ni wanasoka wazuri. Pia na sisi tuna wachezaji wetu."

Kocha wa Barca, Pep Guardiola amekuwa haizungumzii United kwa kuibeza.

Alisema: "Walicheza nusu fainali mechi ya marudiano huku timu nzima ya kwanza ikiwa nje na waliifunga Schalke mabao 4-1.

"Hiyo inaeleza kila kitu unachotaka kujua kuhusu ubora walionao.

"Wana kikosi kizuri chenye timu mbili nzuri na wachezaji wasiokuwa wa kawaida."

Wakati huo huo, kocha huyo aligusia kuhusu habari kama kocha wa Chelsea, Carlo Ancelotti anaweza kutimuliwa endapo watakosa ubingwa msimu huu.

Alisema kitendo hicho kinaweza kumshtua na kumstajabisha na kuongeza kuwa kazi ya ukocha imekuwa na matatizo ya aina hiyo kila wakati.

Kocha huyo alisema kuwa kocha huyo alishwahi kutwaa ubingwa wa Ulaya mara mbili, alitwaa makombe mawili England msimu uliopita, anashangaa kwanini watu wanahoji kuhusu msimu huu.

No comments:

Post a Comment