Na Mwandishi Maalumu, OMR, Istanbul
MAKAMU wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal anatarajia kuhutubia mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya nchi maskini mjini Istnbul, Uturuki, kuuelezea
ulimwengu juu ya nafasi ya Tanzania katikakupambana na umaskini.
Dkt. Bilal atazungumza hayo, huku ikifahamika kuwa Tanzania ilipaswa kuwa
tayari imeondoka katika kundi la nchi 47 ambazo kwa mujibu wa Umoja wa
Mataifa zinatazamwa kama nchi maskini zaidi.
Mkutano huo ulifunguliwa jana na Rais wa Uturuki, Bw. Abdullah Gul kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo ya nchi maskini ulimwenguni.
Rais Gul alisema kuwa ni wakati muafaka kwa nchi tajiri kutumia nafasi yake katika kuwekeza katika nchi maskini kwa kuwa kufanya hivyo si tu kutatanua mtaji wao, bali pia kutatoa fursa kwa nchi maskini kunyanyuka kiuchumi.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki Moon, Rais Gul alisema Uturuki itaendeleza jitihada zake za kusaidia nchi maskini kwa kuzingatia kuwa ni nchi inayounganishwa na mabara mawili, huku pia ikiwa kitovu cha tamaduni mbalimbali kati ya Ulaya na Asia.
Mkutano huo ulianza juzi kwa mikutano ya awali ambapo wabunge kutoka
katika nchi 70 walihudhuria kwa mara ya kwanza na kujadili nafasi ya
mabunge katika kuleta maendeleo katika nchi maskini.
Kushindwa kwa Tanzania kutoka katika kundi hili kunatokana na kuporomoka
kwa uchumi kulikosababishwa na ukame sambamba na muanguko wa uchumi
duniani hali iliyosababisha sekta ya nishati nchini kushindwa kufanya vema
sambamba na mafuta kupanda bei kila kukicha. Hali hii ilitokea wakati
uchumi wa Tanzania ukiwa umeanza kukua na hivyo kushindwa kutulia, hoja
ambayo ni muhimu kwa mataifa kufikiwa ili kuondoka katika kundi hili.
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
alisema, mataifa makubwa yana kazi moja kubwa ya kutimiza ahadi zao
wanazotoa kwa nchi maskini na akayakumbusha mataifa hayo kuwa, nchi
maskini hazina haja ya misaada bali mfumo sawa katika biashara ili nazo
ziweze kujikwamua kwa upatikanaji wa soko lisilo na masharti magumu, yaani
lile la ndani ya nchi hizo na lile la nje.
Bilal umepewa umakamu wa tanzania lakini wenzio wa zanzibar hawapendi muungano. hivi unajisikia vipi unapowakilisha watu wanaochukiana? unajisikia ni mtanzania au mzanzibari? utafanya nini kuwaambia wanzanzibar kuwa unafaidi mapesa yetu?
ReplyDeleteNijibu mzee! tunachomewa vibanda mzee