30 May 2011

CUF kuandamana kupinga mauaji ya kila kona

Na Agnes Mwaijega

CHAMA Cha Wananchi Cuf (CUF) kinaandaa maandamano makubwa kupinga mauaji yanayofanywa na jeshi la polisi kila kona ya nchi ya kuwauwa raia wasio na hatia
yakiwemo mauaji yaliyotokea Jimbo la Urambo kata ya Usinge mkoani Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Katibu wa CUF Bw.Julius Mtatiro alisema matukio hayo ambayo yamekuwa yakijitokeza kila mara yanadhihirisha namna serikali ilivyo dhaifu kwa sababu kila mamlaka inafanya vile inavyotaka.

Pia alisema matukio ya namna hiyo kwa wananchi wasio na hatia kuuwawa,kunyanyaswa, kukamatwa na kubambikiziwa kesi yamekithiri na kinyume cha haki za binadamu .

Pamoja na maandamano hayo chama hicho kimesisitiza kuwa kitachukua hatua zingine ikiwemo kuendelea kulinda haki za kila binadamu na kuwatetea wananchi dhidi ya kila unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya dora vya serikali.

"Tutaandamana hadi tuhakikishe haki ikitendeka kwa wananchi wote bila kubagua,"alisema.

Bw. Mtatiro alisema chama hicho pia kimelaani vikali kukamatwa kwa viongozi wake ambao walitumwa kwenda Urambo kwa ajili ya kufuatilia mauaji na vurugu zinazoendelea katika Jimbo hilo ambazo zimeleta madhara makubwa kwa wafuasi wa CUF na wananchi wa maeneo hayo.

Alisema kinachosikitisha zaidi ni kuwanyima viongozi hao dhamana wakati hawana kosa lolote walilolifanya na kwa taarifa zilizozipata kutoka ndani ya jeshi la polisi ni kuwa kesho watafikishwa mahakamani kubambikiziwa kesi ya kufanya mkutano bila kibali na kusababisha vurugu wakati siyo kweli.

"Jeshi la polisi linatusikitisha sana na tunashindwa kulielewa kabisa, kwa sababu sisi tuliwatuma wajumbe wetu kwenda kufuatilia matukio ya mauaji na watu ambao wamejeruhiwa katika vurugu zilizofanyika katika jimbo hilo ambalo ni la CUF," alisema.

Alisema chama hicho kinashangazwa na kitendo cha jeshi hilo kuwakamata viongozi hao,kwa sababu walipofika katika ofisi ya kata ya Usinge walifanya kazi kubwa ya kuwazuia wanakijiji ambao walipokonywa mifugo yao kufanya vurugu na kuwasihi kulitatua suala hilo kwa njia ya amani.

Aliongeza kuwa  chama hicho kinasikitishwa na kitendo cha Askari wa Maliasili kushirikiana na Jeshi la polisi  kufanya kazi katika makazi ya watu na kuwakamata zaidi ngo'mbe 6,000 na kuwapeleka  makao makuu ya kata ya Usinge kwa madai kwamba wanakikijiji Jimbo la urambo wanachunga mifugo yao katika hifadhi.

Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kata ya usinge kati ya ng'ombe hao 20 wamekufa na wengine wamedhoofika kwa sababu ya kukosa maji na chakula.

"Hii siyo haki wangetaka wangewakamata wanakijiji hao wakiwa na mifugo katika hifadhi na siyo kuwafuata sehemu wanazoishi," alisema.

Alisisitiza kuwa matukio yanatokana na tabia iliyozoeleka kwa vyombo vya dola na askari hao kuvamia wanakijiji,kuwachukulia mifugo yao kwa nguvu na kuanza kuwatoza mamilioni ya fedha ili wawarudishie wahusika mifugo yao.

"Inasikitisha sana kwa sababu ni hivi karibuni tu (Mei 18-20) viongozi wa CUF wilaya ya Geita walikamatwa katika mkutano wa hadhara baada ya polisi kuvunja mkutano huo kwa sababu viongozi wa CCM walikuwa hawataki mkutano huo ufanyike," alisema.

Wafuasi hao ambao wanashikiliwa na jeshi la polisi la Mkoani Tabora ni Mbunge wa viti maalum wa CUF Bi. Magdalena Sakaya,Ofisa wa haki za binadamu,sheria  na wajumbe wa baraza kuu la chama hicho.

Mei 24 mwaka huu asakari wa Maliasili wakishirikiana na askari polisi kuvamia kijiji cha Shela kata ya Ngusa na kuwachukua kwa nguvu ng'ombe zaidi ya 6,000 na kuwapeleka makao makuu ya kata ya Usinge.

5 comments:

  1. Safi sana wana CUF pamoja tutashinda chini ya utawala huu dhalimu wa CCM inayoua raia wake wasio kuwa na hatia.Tuungane pamoja hadi kiileweke.

    ReplyDelete
  2. Mnachekesha sana nyie wakati chadema wakipambana na hali kama hi kule Arusha na Tarime nyie mlisema wanavunja Amani je? CUF wao hawavunji Amani? haki itendeke kwa kila mtu si mwenzako akifanya ww unasema mbaya ww ukifanya unaona inafaa wala si kwamba niko kinyume na wanachotaka kukifanya CUF ila wawe makini saa wakiwasema wenzio wajue swala la kutafuta haki kwa wanachi ni la kila chama cha siasa

    ReplyDelete
  3. MAGWAI A.R CHILENDU
    Hii hali inatisha,mtuhumiwa anapaswa kupelekwa katika mahakama na si kuuwawa kama inavyotokea sasa, kweli safari ya demokrasia itafika nchi hii, tusipoheshimu haki za binaadam kwa kiwango hiki?

    ReplyDelete
  4. Hivi huyu Sheriff Hammad kaishia wapi??!!! Kweli njaa inaua upinzani nchini!! Huyu bwana alikuwa haishi kukusoa serikali lakini baada ya kuhongwa cheo na CCM (kuna tetesi kuwa alishinda uchaguzi Zanzibar) amekuwa kimya kabisa. Yaani upinzani kwakweli ni njaa. Zamani ukisikia CUF inafanya maandamano ujue atayeongoza ni Hammad!! BURE KABISA!!!

    ReplyDelete
  5. inasikitisha sana kuona polisi wanafanya mambo ya kinyama hivi.siamini nchi kuwa kwenye hali kama hii.uongozi mbovu haya ndio matakeo yake ,hawa wshenzi inabidi walipie hizo damu for justice to be done.

    ReplyDelete