Na Rashid Mkwinda,Mbeya
MIILI ya waliokufa kwa ajali ya Basi la Sumry imezidi kutambuliwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Wazazi Meta jijini Mbeya, hivyo kufanya idadi ya
waliokufa katika ajali hiyo kufikia 14.
Baadhi ya waliotambuliwa ni pamoja na mke na mume Kandius Komba ambao kwa mujibu wa maelezo ya ndugu wa Bw. Komba ambaye ni majeruhi katika ajali hiyo aliyelazwa katika
hospitali ya wilaya ya Mbarali Bw. Deodatus Komba alisema kuwa katika safari hiyo alikuwa yeye na shemeji yake.
Alisema safari yao ilikuwa ni kutoka mkoani Arusha kurejea Mbeya.
Wengine waliotambuliwa ni pamoja na Kondakta wa Basi hilo aliyefahamika kwa jina moja la Peter pamoja na dereva wake aliyefahamika kwa jina la Makame Juma.
Miili ya watu wengine waliotambuliwa ni ya Editha Mwaitela(35 na mwanawe Shadrack Idd mwenye umri wa kati ya miaka mitatu na mitano ambapo kwa mujibu wa kaka wa
marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Danford Mwaitela dada yake alikuwa akitokea mjini Arusha anakoishi na alikuwa akielekea kuhani msiba wilayani Kyela.
Wengine ni Martha Mgeta,Burton Joseph, Faraja Mseji huku miili ya watu wawili wa jinsia ya kiume bado haijambuliwa na imehifadhiwa katika hospitali ya wazazi Meta
jijini Mbeya.
Akielezea mtazamo wake juu ya ajali zinazotokea mara kwa mara katika safari ndefu, Mchungaji Danford Mwaitele ambaye ni ndugu wa marehemu Editha na mwanaye
Shadrack alisema kuwa tatizo la madereva kuendesha kwa muda mrefu ni moja ya sababu za ajali hiyo na kuwa madereva wengi hawana ajira bali wanaendesha kama vibarua.
Mchungaji huyo alisema kuwa wamiliki wa mabasi wanajali zaidi maslahi yao bila kujali maisha ya watu na kwamba serikali inatakiwa idhibiti ajali hizi kwa
kuwalazimisha wamiliki kuwa na madereva wawili katika safari ndefu.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Bw. Advocate Nyombi akizungumza kwa njia ya simu alisema kuwa ndugu na jamaa wa marehemu wanaendelea kujitokeza kutambua miili ya
marehemu ambayo imehifadhiwa katika hospitali ya wazazi Meta.
No comments:
Post a Comment