Na Cresensia Kapinga, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Christine Ishengoma amepokea na kuupongeza Kampuni ya Business Times Limited (BTL) kupitia gazeti lake la Majira kwa kubuni mpango
wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali, taasisi, watu binafsi na wananchi kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Amesema kutokana na mpango huo atahakikisha unatekelezwa ili kuharakisha maendeleo ya mkoa na kutekeleza mipango ya maendeleo ya serikali ikiwemo Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2010-2011.
Akizungumza na timu ya Majira kutoka Makao Makuu ofisini kake jana, Dkt. Ishengoma alisema serikali inahitaji ushirikiano mkubwa wa vyombo vya habari na kwamba mpango wa Majira kutoka kuripoti hadi kuwa daraja la maendeleo ya jamii ni fursa ya pekee kwa wana Ruvuma kujiinua kwa kutangaza fursa mbalimbali za mkoa huo.
"Kwa kweli nawashukuru sana kwa kuja mkoani kwetu, nawaomba muendeleze moyo huo, si kuandika habari za ufisadi tu, hata za maendeleo, mambo mazuri yaliyofanywa ni muhimu kwa maendeleo yetu, napongeza sana Majira kwa mpango huu na sisi tumeupokea," alisema Dkt. Ishengoma.
Alisema wananchi wanapenda kusikia pia mambo mazuri yaliyopangwa na serikali kwa ajili yao, mapungufu na mipango ya kurekebisha mapungufu hayo na kwamba iwapo vyombo vya habari vitaendelea kuripoti kwa usahihi utasaidia kuharakisha maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Baadaye akifungua kikao cha Maendeleo ya Mkoa huo (RCC) uliofanyika katika ukumbi wa Songea Club, Dkt. Ishengoma aliagiza halmashauri zote za mkoa huo kutumia sheria ndogo kuhahakikisha dosari zilizosababisha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa darasa la saba zinaondoka na kinapanda mwaka huu.
Alisema yeye akiwa msimamizi mkuu wa mkoa hakuridhishwa hata kidogo na hali ya elimu iliyokwepo mwaka jana hivyo kuagiza kila mmoja kutimiza wajibu wake kukabiliana na hali hiyo kwa manufaa ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Kuhusu kilimo aligiza viongozi wote wa mkoa huo kuongeza kasi ya usimamizi wa pembejeo za kilimo hususan ugawaji wa vocha kujipanga mapema ili kuhakikisha tatizo la usimamizi unafanyika mapema kupunguza kero zilizojitokeza mwaka jana.
"Natoa wito kwa halmashauri zote za wilaya na manispaa kuanza kujipanga mapema sasa ili uratibu wa utambuzi na ugawaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima stahili ufanyike mapema ili kupunguza kero kwa wakulima kwa msimu ujao.
Naagiza kupitia kikao hiki kamati za pembejeo za wilaya na maofisa ugavi kufanya tahmini ya zoezi zima la utambuzi na ugawaji wa pembejeo za ruzuku," alisema Dkt. Ishengoma.
Alikemea tabia ya uharibifu wa mazingira unaofanywa katika mkoa huo hususan ukataji miti ovyo, uchomaji mikaa pamoja na kilimo kisichoendana na uhifadhi wa mazingira hivyo na kutaka wahusika wawajibike kwa kutumia sheria ndogo.
No comments:
Post a Comment