Na Esther Macha, Mbeya
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti Mkoani Mbeya likiwemo la mtu mmoja kuchomwa kisu tumboni na mkwewe hatimaye utumbo wake
kumwagika nje huku mwingine akigongwa na gari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Bw. Advocate Nyombi alisema tukio la kwanza lilitokea katika wilaya ya Chunya likimhusisha Msenegali Mwakalambile mkazi wa Kijiji cha Kibaoni wilayani Chunya ambaye alimchoma kisu cha tumbo mkwewe Ponali Mwalingo kutokana na ugomvi uliotokea kati yao.
Kamanda Nyombi alisema chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliozuka kati ya ndugu hao baada ya Msenegali Mwakalambile kwenda nyumbani kwa marehemu Ponali Mwalingo kutaka kumchukua mkewe aitwaye Bertha Ponali (36) na kwa lengo la kurudiana naye baada ya kutengana kwa muda mrefu
Akielezea zaidi tukio hilo Kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea Mei 29 mwaka huu majira ya saa 12 Jioni na kabla marehemu hajakata roho alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya na kulazwa kisha akakata roho.
Hata hivyo Mke wa mtuhumiwa Msenegali Mwakalambile, Bertha Ponali alijeruhiwa katika sakata hilo huku mtuhumiwa akitokomea kusikojulikana na jeshi la polisi mkoani Mbeya linaendelea kumtafuta kwa kesi hiyo ambayo jalada lake limefunguliwa polisi kwa namba CHU/IR/392/2011.
Wakati huo huo Mkazi wa Chimala wilayani mbarali Bw.Joseph Mkwama amekufa baada ya kugongwa na gari ambalo halikujulikana katika eneo la Godown Chimala akiwa anaendesha Baiskeli.
No comments:
Post a Comment