Na Pendo Mtibuche, Dodoma
SERIKALI imeanza kutekeleza mpango wa kupunguza idadi ya akaunti za benki zinazoendeshwa na Mamlaka za serikali za mitaa kutoka wastani wa akaunti
30 kwa kila mamlaka hadi kufikia akaunti 6 lengo likiwa ni kuimarisha matumizi ya fedha za umma.
Tayari hatua za kusimika Mfumo wa kompyuta ya usimamizi wa fedha umesimikwa serikali kuu na katika mamlaka zote za serikali za mitaa kwa kuunganishwa kupitia mkongo wa Taifa unaosimamiwa na shirika la simu (TTCL).
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu Tamisemi, Bw. Parkishard Mkongwa wakati akizungumza na waweka hazina katika mafunzo ya Kikanda yanayoendelea mkoani hapa juu ya mfumo mzima wa usimamizi wa fedha kwenye mamlaka za serikali za mitaa nchini.
Bw. Mkongwa alisema kuwa katika utaratibu huo shughuli zote za usimamizi wa mfumo zitafanyika katika ngazi ya Wizara ya Tamisemi wakati mamlaka za serikali za mitaa zenyewe zitabaki na jukumu la utendaji wa kila siku ikiwa ni pamoja na kuhakikisha malipo ya fedha yanaingizwa kwenye mfumo huo kwa usahihi.
Hata hivyo alisema kuwa, kuanzishwa kwa mfumo huo kutasaidia kuondokana na tatizo la hati chafu kwani Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi itahusika na kusimamia mfumo huo kwenye kompyuta kuu zitakazosimikwa Dodoma na kuziunganisha mamlaka zote kwenye miundombinu kwa kutumia mkongo wa mawasiliano.
Alisema kuwa mikoa itapewa fursa ya kuendelea kuzisimamia mamlaka hizo kwa kuunganishwa kwenye mfumo huo kwa kupitia mkongo huo na hivyo kuweza kuona malipo ynayoendeshwa na mamlaka zilizoko chini yake.
Hadi sasa jumla ya wahasibu 266 wameshapewa mafunzo hayo kwa wastani wa wahasibu wawili kwa kila halamshauri ambapo kwa upande wa waweka hazina mafunzo ya mfumo huo yameanza na yanatolewa katika kanda ya Kati, Kaskazini na kanda ya Mashariki.
No comments:
Post a Comment