24 April 2011

Vigog CCM Kahama wagoma kujivua Gamba

Na Suleiman Abeid, Kahama
 
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wimbi la kujivua ‘gamba’ ndani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) limechukua sura mpya baada ya
 viongozi wa chama hicho  wilayani
Kahama mkoani Shinyanga kugoma kujivua gamba na kuwashinikiza kwanza viongozi wa
ngazi za matawi na kata waanze kufanya hivyo wao.
 
Hali hiyo ilijitokeza mapema wiki hii katika kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya
CCM ya wilaya ya Kahama kilichoitishwa kwa lengo la kupongeza hatua ya Halmashauri
Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) kuamua kuanza kujivua gamba kwa kuwatosa baadhi ya
viongozi wake wakuu wa kitaifa ikiwa na lengo la kujisafisha.
 
Hata hivyo katika hali ambayo iliwashangaza baadhi ya wajumbe ni kitendo cha
viongozi wa wilaya waliotakiwa kujivua gamba wakidaiwa kuchangia matokeo mabaya ya
uchaguzi yaliyosababisha CCM kupoteza viti katika baadhi ya kata za wilaya hiyo
kugoma kujiuzulu na kuwashinikiza viongozi wa ngazi za matawi na kata waanze kufanya
hivyo.
 
Viongozi hao wa wilaya walidai hawawezi kuwajibika kutokana na kwamba watu
waliochangia CCM ipoteze baadhi ya kata kwenye nafasi za udiwani katika uchaguzi
mkuu uliopita ni viongozi wa matawi na kata na hivyo ndiyo wanaopaswa kuvuliwa
magamba badala ya wao.
 
Mvutano huo ulisababisha Katibu wa Uchumi na Fedha kutoka Kata ya  Bulungwa, Bw.John Kapaya asimame na kuwahoji viongozi wa wilaya ni sababu zipi zilizosababisha
waitishe kikao hicho kipindi hiki ambacho moja ya agenda zake ni kufanya tathimini
ya uchaguzi mkuu uliopita wakati tayari tathimini ya kimkoa iliishafanyika na
kutumwa makao makuu.
 
Kutokana na hali hiyo, Bw. Kapaya alisema kuna kila sababu za wazi kwa viongozi wa
ngazi ya wilaya kujivua gamba kwa kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na udhaifu mkubwa
waliouonesha katika utendaji wao wa kazi hali iliyosababisha matokeo mabaya kwa CCM
katika uchaguzi mkuu uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.
 
Mwanachama mwingine Bw. Boniface Paul mkazi wa kitongoji cha Nyakato wilayani Kahama
alisema dhambi iliyofanywa na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya haipaswi kusameheka
hivyo wanastahili kujivua gamba wao wenyewe bila kushinikizwa na mtu.
 
Bw. Paul alisema tangu kipindi cha upigaji wa kura za maoni ndani ya CCM viongozi
hao hawakuonesha uadilifu na kuzingatia maadili ya uongozi ndani ya chama hivyo ni
wazi suala la kujivua gamba kwao halikwepeki kwa hivi sasa.
 
Hata hivyo palijitokeza kundi la pili ambalo lilipinga kwa nguvu zote shinikizo
lililowataka viongozi wa wilaya kujivua gamba na kudai kwamba kama ni suala la CCM
kupoteza viti vya udiwani lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa ngazi ya
matawi na kata.
 
Mmoja wa wasemaji katika kundi hilo lililowatetea viongozi wa wilaya alisema
hapakuwa na haja ya viongozi hao kujiuzulu na kusisitiza kufanyika kwa suluhu na
kusameheana kati yao baada ya kubaini kila upande una makosa yake.
 
Mwanachama huyo alishauri kuzingatiwa kwa ushauri  wa kuvumiliana uliotolewa na
mwenyekiti mstaafu wa CCM wilaya, Bw. Edward Msoma ambaye alisema kila mwanachama
ana dhambi zake kwa namna moja ama nyingine ambapo wengine katika kipindi cha
uchaguzi mkuu hawakujitoa katika kukipigania chama huku wakijihusisha zaidi na
vitendo vya rushwa.
 
Naye mwanachama mwingine Bi. Kundi Masanja alisema kama ni suala la kuwataka
viongozi wajivue gamba kutokana na matokeo mabovu yaliyopita itakuwa ni kuwaonea
kwani kila mwanachama dhambi hiyo anastahili kuibeba kwa kudiriki kushiriki rushwa
wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu kwa kutoa au kupokea rushwa.
 
“Jamani tusihukumiane kwa masuala ya rushwa, sote tumeshiriki haswa kwa hawa
viongozi wa kuchaguliwa, tumeshiriki nao kikamilifu katika masuala ya rushwa, kama
kuna anaedai hakutoa rushwa, basi asimame hadharani athibitishe ukweli wake kwa
kushika kitabu cha mungu kwamba hakufanya hivyo,” alieleza Bi. Masanja.
 
Bi. Masanja alisema hakuna sababu ya kutafutana uchawi kwa mapungufu yaliyojitokeza, bali kila kiongozi anayeamini kuwa alikwenda kinyume wakati wa kipindi cha uchaguzi basi ni vyema akatubu dhambi alizozifanya na kula kiapo katika nafsi yake kuwa anarejea katika maadili yaliyoasisiwa na waasisi wa chama hicho.
 
Kutokana na hali hiyo hapakuwa na kiongozi hata mmoja katika kikao hicho aliyekubali kujiuzulu katika wadhifa wake hali inayoashiria hivi sasa chama kuwa katika wakati mgumu kutokana na kutokea makundi mawili yanayohasimiana na kutishia
uhai wa chama hicho katika wilaya hiyo.
 

No comments:

Post a Comment