24 April 2011

Babu Ajitoa kuondoa msongamano Pasaka

*Alazimika kugawa kikombe siku ya mapumziko
*Ahudumia wagonjwa na kupunguza magari 300
*Madiwani:Fedha za ukimwi zipelekwe Loliondo


Na Said Njuki, Arusha
KUVUNJWA kwa taratibu za safari za kwenda kwa Mchungaji Ambilikile Masapila wa Samunge Loliondo wilayani Ngorongoro na wakorofi wachache katika vituo vya kuratibu safari hizo kumemlazima mchungaji huyo kuendelea kutoa tiba hiyo jana.
Mchungaji huyo alilazimika kusitisha mapumziko yake ya Pasaka aliyoanza juzi na kuamua kutoa tiba hiyo akiwahurumia mamia ya
wagonjwa waliokwama kijijini hapo kwa siku kadhaa wakisubiria tiba na kukutwa na Pasaka wakiwa katika foleni.
Taratibu hizo zinadaiwa kuvunjwa na baadhi ya waratibu wa safari hizo hususan kituo cha Bunda kinachoratibu wagonjwa kutoka Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.
Vituo vingine vipo Babati mkoani Manyara na Arusha ambapo kwa kiasi kikubwa inadaiwa vilitekeleza agizo la Serikali kwamba
Jumanne iliyopita ilikuwa ndiyo siku ya mwisho ya kuruhusu magari zaidi kuelekea huko.
akizungumza kwa njia ya simu Msaidizi wa Babu Bw. Jackson Dudui jana alisema babu amelazimika kutoa huduma hiyo jana kwa kuwaonea huruma wagonjwa waliobaki porini wakisubiria tiba hivyo haoni sababu ya kupumzika huku akiwaona wagonjwa wakiteseka kwa kumsubiria.
"Tumelazimika kufanya kazi leo na hata kesho kutwa Jumatatu tutafanya kwa kuwa babu anawaonea huruma wagonjwa waliokwishafika hapa halafu wabaki siku kadhaa wakisubiria huduma huku yeye akila
Pasaka, ameshindwa,"alisema msaidizi huyo.
Aliongeza kuwa hadi jana saa 6 tayari babu aliondoa magari zaidi ya 300
na alitarajia kufanya kazi hadi jioni huenda akazimaliza zote.

Naye Yusuph Mussa anaripoti kuwa baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi wamesema fedha zilizotengwa kwenye Bajeti ya halmashauri hiyo sh. milioni 50.3 kwa mwaka wa fedha 2011/12 kwa ajili ya kutoa semina na uratibu kwa waathirika wa ukimwi, zitumike kuwapeleka waathirika hao kwa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Masapila.

Walitoa ushauri huo hivi karibuni wakati wa kujadili mapendekezo ya bajeti ya
halmashauri hiyo, ambapo walisema wameona kuna mlolongo mrefu kwenye fedha hizo
ikiwemo semina, watoa mada kugawana posho, hivyo wakataka njia ya mkato ambayo
inawalenga waathirika wenyewe kwa kuwapeleka kwa ‘Babu’.

“Nimeiona bajeti hii, lakini kuna kipengele cha maambukizi ya ukimwi ambapo kuna
semina kwa ajili ya waathirika na wagonjwa wa ukimwi. Napendekeza, badala ya fedha
hizi kutumika kwa semina, warsha na makongamano na watu kulipana posho ni vizuri
fedha hizo zikatumika kuwasafirisha wagonjwa wa ukimwi kwenda kwa Babu, Loliondo”
alisema Diwani wa Kata ya Masagaru Bw. Mohamed Makengwa.

Mbunge wa Kilindi Bi. Beatrice Shelukindo alisema kikombe cha Babu kinaponyesha,
lakini ni mpaka mtu awe na imani, kwa kuwa yeye ni shuhuda baada ya kunywa kikombe
hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Mussa Semdoe alisema itabidi hilo la
kwenda Loliondo walijadili kwa kina baada ya kikao hicho kumalizika, kwa vile linaweza
kuwasaidia wagonjwa wengi,na kwamba anaamini kuna madiwani na watumishi wa halmashauri
ambao baadhi yao wameathirika.

Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Dkt. Joseph Chabai alisema
madiwani hawawezi kutengua bajeti hiyo kwa kupeleka wagonjwa kwa Babu kwa vile yeye
hafahamiki na jopo la wafamasia kama dawa yake ni halali na inaponyesha.
“Hatuwezi kubadilisha matumizi ya fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa waathirika na
wagonjwa wa ukimwi na kuanza kusafirisha watu kuwapeleka Loliondo. Tiba ya Babu bado
haijathibitishwa na Serikali kama inaponya, na pia Babu hajatambulika na wafamasia
kama naye ni mmoja wao” alisema Dkt. Chabai.

Baadhi ya kazi zitakazofanywa na sh. milioni 50.3 za ukimwi ni kufanya semina ya
siku tano kwa watu 20 wanaoishi na virusi vya UKIMWI ili wazijue haki zao, kusaidia
vikundi 12 vya watu wanaoishi na virusi kuanzisha miradi, kusaidia klabu 15 katika
shule za msingi kuhamasisha mapambano dhidi ya ukimwi.
Nyingine ni kugharamia matengenezo ya pikipiki DFP 3322 ya shughuli za ukimwi na
ununuzi wa mafuta, gharama za uendeshaji wa ofisi ya Mratibu wa ukimwi Wilaya, kugharamia vikao vya Kamati ya ukimwi ya Wilaya na kufanya ufuatiliaji wa Kamati za
ukimwi za vijiji vitano.

No comments:

Post a Comment