24 April 2011

Kampuni ya DataVision yapata Zawadi ya Pasaka wasiojiweza

Na Mwandishi Maalum

KAMPUNI ya DataVision International Limited imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa kituo cha wasiojiweza cha Kimbangulile Support Group kilichopo kata ya
 Mianzini, eneo la Mbagala Rangi Tatu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Meneja Masoko na Mahusiano wa kampuni hiyo, Bi. Teddy Qirtu alisema kampuni yao inajishughulisha na masuala ya utafiti, takwimu, menejimenti na mifumo ya teknolojia ya mawasiliano lakini imejikuta ina wajibu
wa kuisadia jamii hasa watoto wenye mahitaji maalum.

Alisema uamuzi wa kukitafuta kituo hicho na kukisaidia unatokana na mfumo wa kuendeleza jamii (growing people) na kutimiza wanayoyasema (walking the talk) ambao kampuni hiyo imejiwekea chini wa mpango wake wa huduma kwa jamii (Corporate Social
Responsibility -CSR)

“Nia yetu ni kutaka kukua na watoto wa kikundi ili kesho na kesho kutwa nanyi mjikute mko sehemu fulani... tutapenda kuona watoto kutoka hapa wakiwa wachumi, walimu, watangazaji au madaktari,” alisema Bi. Qirtu.

“Tumeamua kwamba Pasaka yetu iwe ni kwa ajili ya kikundi cha Kimbangulile... tunatambua kwamba kikundi kina mahitaji mbalimbali nasi tumejichangisha na kuamua kutoa msaada wa vyakula ili watoto wa hapa wajisiki kuna watu wanaowapenda na kwajali,”
alisema.

Misaada iliyokabidhiwa ni kilo 100 za sukari, kilo 100 za mchele, kilo 50 za unga wa mahindi, kilo 50 za maharage, katini nne za sabuni, katoni ... za juisi na katoni ... za biskuti vyote vikiwa na thamani ya sh. 500,000.

Akipokea msaada huo, Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Bibi Leokardia Mchau alishukuru kwa msaada huo na kubainisha kituo hicho lengo lake kuu lilikuwa ni kusaidia watoto wa mtaa wao wapate matunzo, elimu na waache kuzurura hovyo.

Alisema wanahitaji maombi zaidi ili wamudu jukumu la malezi kwani wana watoto 20 ambao wamefanikiwa kuwaingiza katika shule za msingi zilizo eneo la jirani na kituo chao.
Alizitaja shule hizo kuwa ni Mchikichini, Upendo Kongowe na Mbagala Rangi Tatu.

Naye Katibu wa kikundi hicho, Bi. Mary Mbega alisema hivi sasa kikundi chao kinahudumia watoto 64 ambao saba kati yao ni walemavu wa viungo, 30 ni yatima na 27 wanaishi katika mazingira magumu.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Bw. Abdul Kessy ambaye pia ni mlezi wa kituo hicho aliomba wafadhili wengine wajitokeze ili wawasaidie kukabiliana na changamoto
ya kununua eneo la mbande na kujenga kituo maalum kwa ajili ya watoto hao.

Alisema katika kushirikiana na akinamama hao, amekuwa akilazimika kuingilia kati kuandika barua ili watoto wasifukuzwe shule kwa kukosa kulipa michango ya walinzi au
kukosa madaftari.

No comments:

Post a Comment