18 April 2011

TP Mazembe yazidi kuvuna Simba

*Ochan naye atua Lubumbashi

Na Zahoro Mlanzi

KIUNGO wa timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' na Simba, Parick Ochan amemfuata mchezaji mwenzake, Mbwana Samatta kwa mabingwa wa Afrika, TP Mazembe
kwa mkataba wa miaka mitano.

Ochan atakuwa mchezaji wa pili kunyakuliwa na mabingwa hao wa Afrika baada ya Samatta, wiki iliyopita kusajiliwa na klabu hiyo kwa ada ya uhamisho wa sh. milioni 100.

Kwa mujibu wa taarifa ya Klabu ya TP Mazembe, ilieleza kwamba wachezaji hao wote kwa pamoja walisainiwa tangu Alhamisi iliyopita katika hoteli ya Movenpick Royal Palm jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba TP Mazembe walikuja Dar es Salaam zaidi ya mara mbili kuzungumza na viongozi wa Simba, huku wakiongozwa na Rais wa timu hiyo, Moses Katumbi na Meneja Frederick Kitenge  Kinkumba, ambapo baada ya kukamilisha suala hilo walifungua mvinyo na kusherehekea.

"Chaguo la kwanza lilikuwa ni kwa Mganda Patrick Ochan, ambaye walipoumana na timu hiyo ya Simba alipokuwa amevaa jezi namba 10 waliridhishwa na kiwango chake ndipo walipotuma wakala wao aanze kumfuatilia," ilieleza sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza zaidi kwamba, Ochan tayari alishakwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na alikaa kwa siku nne ambapo alionana na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Lamine N'Diaye.

Chaguo la pili lilikuwa kwa mshambuliaji Samatta ambaye wakati wa kusaini mkataba Movenpick, alikuwepo na kaka yake, Ali Samatta na baba yake Mzee Samatta wakisherehekea kusaini mkataba huo.

Samatta na familia yake wanatarajiwa kutua Lubumbashi keshokutwa, akiambatana na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' kwa kukamilisha makubaliano ya mwisho.

Taarifa hiyo ilifafanua zaidi, licha ya wachezaji hao kusaini mkataba wa miaka mitano, lakini ada ya uhamisho bado haijawekwa wazi mpaka sasa na itawekwa wazi baada ya kukamilisha kila kitu keshokutwa.

Alipotafutwa Kaburu kuzungumzia suala hilo, alikiri kweli Ochan kutakiwa na TP Mazembe na kwamba wiki ijayo atakwenda nchini humo kufanya majaribio.

No comments:

Post a Comment