Na Amina Athumani
BINGWA wa Dunia wa kickboxing, Japhet Kaseba ametangaza kuachana na mchezo wa ngumi na kujikita zaidi katika kuendeleza vipaji vya kickboxing kwa vijana.Kaseba
amefikia hatua hiyo baada ya kubondwa na Mada Maugo katika pambano lililofanyika juzi katika Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
Maugo alishinda pambano hilo la uzito wa kg. 72 mara baada ya Kaseba kuingia ulingoni akiwa amevua glovs katika raundi ya saba ya pambano hilo, ikiwa imepaki raundi moja mchezo kumalizika ambapo mwamuzi John Chagu akamtangaza Maugo kuwa mshindi wa pambano hilo.
Akizungumza na mwandishi wetu Dar es Salaam jana, Kaseba alisema endapo ataendelea kucheza mchezo huo lawama zitakuwa haziishi na kwamba ni bora awe nje ya ulingo, ili aweze kuendeleza vipaji vya vijana zaidi.
"Mchezo ulikuwa mzuri, ila tatizo ni kwamba viongozi wa ngumi hapa nchini si mzuri wamekaa zaidi kichuki na kickboxing na ndiyo maana wamekuwa wakiweka jitihada za kuhakikisha ushindi unakwenda kwenye ngumi.
"Nilipokuwa nikimwangusha Maugo, nilikuwa sihesabiwi pointi lakini mimi nilipocheza faulo moja 'kumkata mtama' badala ya kunionya wananipa adhabu hii ni hatari na kamwe hatutafika kama itaendelea kuwa hivi," alisema Kaseba.
Katika pambano hilo ambalo pia kulikuwepo na mapambano mengine ya utangulizi, ikiwa ni pamoja na kumtafuta bingwa wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania(TPBO) ambapo, Yohana Robart alitangazwa bingwa wa mkanda huo baada ya kumtwanga Saidi Zungu kwa KO raundi ya nne.
No comments:
Post a Comment