18 April 2011

Serikali yadaiwa kulizwa matrekta ya Kilimo Kwanza

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI inatarajiwa kuingia hasara kubwa katika kipindi kifupi kijacho kutokana na kununua matrekta madogo kutoka Pakistan ambayo hayana ubora.Hasara hiyo
inayotarajiwa kuitikisa serikali inakuja kipindi ambacho tayari Kamati ya Bunge Kilimo na Ushirika, imeibua tuhuma nzito za ufisadi katika ununuzi wa matrekta hayo ya Kilimo Kwanza ambayo hayana uwezo wa kulima ardhi ya Tanzania.

Kwa mujibu wa mmoja wa wabunge wa Kamati ya Biashara na Viwanda, hasara hiyo inagusa zaidi halmashauri ambako matrekta hayo yamesambaa kutokana na unafuu wa bei kwa kupitia kampuni za kijanja, huku wakala mkuu wa kuingiza matrekta halali nchini, Kampuni ya FMD East Africa, ikiachwa bila kuhusishwa.

Alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu uchakachuaji huo, Meneja Mkuu wa FMD (EA) Ltd, Bw. Robley Fergus alisema ni kweli wakulima wengi wanapotoshwa na kuwepo huku kwa matreka feki katika soko si hapa Tanzania tu, bali Afrika Mashariki yote, ambayo yana nembo ya Massey Ferguson Millat.

Fergus alifafanua kwamba, matrekta ya ukweli ya aina ya Massey Ferguson ambayo awali yalikuwa yanatengenezwa Uingereza kwa sasa yanatoka Brazil, Ufaransa na Finland na katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, wakala wake pekee ni kampuni yake, FMD (EA) Ltd ambao pia ndio wauzaji na wasambazaji wa MF pamoja na vipuri vyake.

Alisema matrekta hayo aina ya Massey Ferguso mbali na kuwa chini ya kiwango, yalitengenezwa kwa ajili ya ardhi ya Pakistan ambayo ni tofauti na ile ya Afrika ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, leseni ya utengenezaji wa matrekta hayo ilitolewa kwa Kampuni ya Millat Tractors Ltd ya Pakistan zaidi ya miaka 30 iliyopita, kwa masharti yatumike katika soko la ndani la Pakistan na yasiuzwe nje ya nchi hiyo kitu ambacho AGCO ambao walikuwa watengenezaji wakuu wa matrekta hayo wanaaamini hakitendewi na Millat.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Cyril Chami, ambaye wizara yake inadhamana na ubora wa bidhaa, alipoulizwa kuhusu kuwepo matrekta hayo chini ya viwango, alisema hakuna malalamiko ya matrekta hayo kuwa feki, bali kilichopo ni kuwa yanashindwa kulima katika ardhi ya Tanzania.

Dkt. Chami alisema wanaoweza kutoa majibu mazuri ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, lakini pia yeye yuko yatai kuagiza uchunguzi wa matrekta hayo hata leo, ili kuthibitisha ubora wake.

Imebainika pia katika uchunguzi huo kwamba, matrekta  hayo ambayo awali pia yalitengenezwa na Massey, asilimia kubwa ya vipuri vyake kwa sasa vimechakachuliwa na havifanani na vile vya awali, hivyo havipatikani hapa nchini na watengenezaji hawaruhusiwi kuviuza nje ya Pakistan kutokana na kubanwa na mkataba.

Uchunguzi unaonyesha zaidi kwamba, watengenezaji wa matrekta hayo kutoka Pakistan nao wamethibitisha kutokuwaruhusu wakala wake kuyauza nje na kutamka baya hawahusiki kutoa huduma yoyote baada ya mauzo nje ya Pakistan.

Uchunguzi huo wa kinyaraka unaonyesha kwamba, katika kutekeleza mpango wa Kiilimo kwanza, halmashauri karibu zote zimenunua matrekta madogo ya mkono (Power Tillers) kwa wingi kwa ajili ya kuwauzia wakulima na vikundi vya pamoja vya ushirika.

Lakini, uchunguzi huo unaonyesha kwamba katika baadhi ya wilaya wakulima wengi wameshindwa kuyatumia kutokana na kushindwa kuhimili aina ya ardhi katika sehemu nyingi za nchi.

Katika uchunguzi huo imethibitisha kwamba, upo pia udanganyifu katika aina na nchi, kuhusu mahali matrekta hayo yalikotengenezwa ambapo uchunguzi umebaini mengine yameagizwa kutoka Japan lakini ukichunguza ni nembo tu inaashiria hivyo.

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Magembe, alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuathirika kwa programu ya Kilimo Kwanza, alisema angetoa ufafanuzi baadaye.

1 comment: