*Paroko ahimiza ujasiri kukemea maovu
Grace Michael, Dar na Heckton Chuwa, Moshi
WAKATI mwaka huu Tanzania inaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kupata uhuru wake, imeelezwa kuwa itaendelea kuwa nchi ya chini kimaendeleo
ikilinganishwa na nchi nyingine duniani kutokana na watu wake kutopenda kufanya kazi na kuathiriwa na 'vilema vitatu'.
Tahadhari hiyo imetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mhashamu Isaac Amani, wakati akitoa salamu zake za Pasaka katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme, mjini Moshi, jana.
Alivitaja vilema hivyo kuwa ni ulevi wa kupindukia, kuishi kinyumba na utandawazi.
Alisema wengi wa Watanzania bado wako vijiweni, hawataki kufanya kazi na kwamba tabia hiyo imesababisha kidogo kinachopatikana kutokana na wachache wanaojituma, kitumiwe kwa taabu na watu wengi, wengi wao wakiwa ni wale wasiotaka kujituma.
Askofu Amani alisema suala hilo na mambo mengine yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya nchi, na kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na ulevi wa kupindukia ambao alisema ni moja ya vilema vitatu ambavyo vimelikumba Taifa la Tanzania katika wakati huu linapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru wake.
“Kuna vilema vinavyopatikana kwa ajali, kuzaliwa na vingine vya kujitakia, hivi vya kujitakia ni pamoja na ulevi wa kupindukia, kuishi kinyumba na utandawazi, kwa kweli hivi vitatu vinaelekea kuipeleka nchi yetu pabaya,” alisema.
Alisema ulevi wa kupindukia umewamaliza na unaendelea kuwamaliza watu wengi haswa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa ambapo alisema kuna baadhi ya viongozi na wananchi ambao si waaminifu na ambao wamekuwa wakiyaona haya na kuyafungia macho.
“Pombe hizi zinauzwa katika maeneo tunayokaa, baadhi ya viongozi wanayajua haya na kuyaona lakini wanayafumbia macho hii imesababisha watu wengi kutokufanya kazi kutokana na nguvu kazi ya Taifa kumalizwa na ulevi wa gongo tena katika kipindi hiki ambapo Taifa linaadhimisha Jubilei muhimu ya Uhuru wake,” alisema.
Kuhusu kuishi kinyumba, askofu huyo alisema kuwa tabia hiyo imekithiri miongoni mwa wakristu wengi na kwamba umepora haki na uhalali wa ndoa kama alivyoelekeza Mwenyezi Mungu, ambapo alisema kitendo hicho kimekuwa mfano mbaya katika maisha ya kila siku, kiasi cha hata watoto na vijana kuona ya kuwa ni jambo la kawaida katika maisha.
Aidha Askofu Amani alisema utandawazi ni kilema kingine ambacho kinaiweka nchi mahali pabaya na kwamba tayari umeshaanza kuwadhuru Watanzania wengi wakiwemo watoto wadogo.
“Mfano mzuri ni matumizi ya simu za mkononi ambazo kwa sasa zinatumika vibaya, ambapo watu wanazitumia kwa kutumiana ujumbe wa matusi, vitisho, uchochezi, kupanga ujambazi na mambo ya fitina, hivyo kupoteza maana halisi ya matumizi ya vyombo hivi muhimu ambayo vililengwa kurahisisha mawasiliano,” alisema.
Aliagiza ya kuwa wakati Taifa likiendelea kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wake kuwe kunafanyika sala maalumu ya kuliombea taifa kila siku kila baada ya ibada, katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu na mashirika yote
ya kikatoliki jimboni humo hadi kilele cha sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, zinazotarajiwa kufanyika Desemba, mwaka huu.
Ujasiri wa kukemea maovu
Waumini wa Kanisa Katoliki na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kuiombea nchi ili ipate watu wenye ujasiri wa kukemea maovu nchini, ukiwemo ufisadi, kwa kuwa watu wengi wameshindwa kusimamia haki kutokana na kufungwa midomo yao kwa kununuliwa.
Kutokana na baadhi ya watu kushindwa kusimamia haki kumewafanya kushindwa kutofautisha dhambi na isiyo dhambi hatua inayokwamisha hata kumwogopa Mungu.
Alikwenda mbali zaidi na kuwakumbusha waumini utendaji kazi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage, ambapo alisema kuwa kutokana na kuwa na moyo wa kuwatumikia kwa dhati Watanzania ilifika mahali hata akaisahau familia yake na ikabaki ya kawaida sana ambayo haina tofauti na familia za wananchi wa kawaida.
"Baba wa Taifa ilifika mahali akawashangaa hata wanaogombania kwenda Ikulu, alihoji sana na ndio maana familia yake ni ya kawaida tofauti na watoto wa viongozi wa siku hizi ambao wana fedha kibao na sijui wanazitoa wapi, hivyo kama waumini tunatakiwa kuiombea nchi yetu amani," alisema.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam kwenye mkesha wa pasaka na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kitunda, Padri Maximilian Wambura wakati akitoa mahubiri katika ibada hiyo.
"Katika kipindi hiki tuna kila haja ya kuliombea taifa letu amani...viongozi wetu wanatakiwa kuombewa sana kwa kuwa hata magamba wanayodai kujivua hakuna kitu chochote, imefika mahali watu wameshindwa hata kutofautisha dhambi na neema kwa kuwa muda wote wako ndani ya dhambi na wengine wameshindwa kusimamia ukweli kutokana na midomo yao kufungwa na plasta," alisema Paroko Wambura.
Ibada hiyo ya pasaka pia ilikuwa na matukio mbalimbali yakiwemo ya baadhi ya waumini kuokea sakaramenti za ndoa, ubatizo na kipaimara ambao nao aliwataka kudumu katika imani yao na kuachana na tabia ya kuhama hama makanisa kwa kuwa kufanya hivyo ni kukwepa kubeba misalaba yao.
Alisema kuwa ukwepaji wa kila mmoja kubeba msalaba wake umewafanya baadhi ya wananchi kudanganyika kutokana na matatizo yanayowakabili yakiwemo maradhi, kufarakana kwa ndoa, tamaa ya mali yanayofanya kujikuta wakihangaika na kubadili makanisa kwa kukimbilia mengine ambayo yameanzishwa kwa tamaa za kifedha.
"Kuna wimbi la watu kuhama hama makanisa lakini wengi ukiwachunguza utabaini wamekata tamaa, wapo wanaotaka watajirike kwa kuombewa, wapo wanaokwenda kwa kusumbuliwa na maradhi lakini Mungu wetu anasema kama unaumwa nenda hospitali na ndio maana kawaweka madaktari na kama unahitaji mali unatakiwa ufanye kazi sana...pamoja na kuwepo kwa watu ambao wamepewa nguvu za kiroho lakini kama muumini unatakiwa kuubeba msalaba wako," alisema.
Akiwaasa wanandoa aliwataka kuwa wavumilivu na kutokuwa na makuu kwa wenza wao kwa kuwa siri ya ndoa ni uvumilivu.
"Ndoa nyingi zinasambaratika kwa kuwa wengi wanataka makuu, wanataka kulipiza visasi kwa wenzao wao na matokeo yake huwa ni mabaya zaidi, hivyo kama ndani ya ndoa mmetofautiana mnatakiwa kuwaona hata wazazi na mkishindwa zipo taratibu hata za kumwona padri ili awasaidie kumaliza tatizo lenu," alisema.
No comments:
Post a Comment