25 April 2011

Askofu aonya katiba mpya

*Asema isiandikwe kama ilani za vyama
*Ataka kila jambo lijadiliwe kwa kina


Na Tumaini Makene

WAKATI mchakato wa namna ya kuratibu maoni ya uandikwaji wa katiba mpya ukisubiri sheria ya bunge, wanasiasa walioko
madarakani na wale wa upinzani wametakiwa kuacha kuutaifisha kwa kuufanya sawa na uandishi wa ilani za vyama vyao vya siasa.

Imeelezwa kuwa katiba, ambayo ni sheria mama ya nchi haiwezi kuwa mali ya chama chochote kile cha siasa, pia haipaswi kuandikwa kwa ajili ya kuwasaidia wapinzani kuingia madarakani wala si kwa ajili ya kuwalinda walioko madarakani kuwazuia wapinzani wasiingie kuongoza nchi.

Pia imeelezwa kuwa katika kufikia mchakato huo, haitakuwa sahihi kuitupa katiba ya sasa, kwani 'haikuwa kitabu cha shetani', kwani ina mambo mengi mazuri ambayo Watanzania hawana budi kuyabakiza na kuyaendeleza katika katiba mpya.

Hayo yamesemwa jana katika ibada ya kitaifa ya Sikukuu ya Pasaka, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, ambapo katika ujumbe wake Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, aliwataka Watanzania kuwa na nia njema na umakini katika mchakato wa kuipata katiba mpya.

"Nchi yetu sasa hivi iko katika wakati muhimu sana katika historia na ustawi wa nchi yetu, tunataka kuandika katiba mpya, katiba ni sheria mama ya nchi yeyote ile. Wito wangu kwetu sisi sote, maana ni kitu ambacho kinamgusa kila mtu.

"Mimi kitanigusa katika uhuru wa kuhubiri haya ninayohubiri, pia kitanigusa kama raia na kila kitu, hivyo kila mmoja anahusika. Wito wangu ni kwamba, kitu ambacho...dalili za mwanzoni zilizojitokeza, tunataka kuandika katiba ya nchi kana kwamba tunaandika ilani za vyama vyetu vya siasa.

"Hili limeshaanza kuonekana, katiba sio mali ya chama chochote cha siasa, katiba ni sheria mama ya sisi sote, tukianza kuvutana kwa tofauti zetu za kisiasa kana kwamba tunaandika ilani za vyama vyetu vya kisiasa tunaanza kwa msingi uliokuwa mbovu katika kupata sheria mama ya nchi yetu," alisema Askofu Nzigilwa.

Aliwataka wanasiasa kuacha kuuteka mjadala wa uratibu na hatimaye mchakato wa uandikaji katiba mpya, kwa maslahi ya vyama vyao vya kisiasa, akisema kuwa katiba ya nchi haipaswi kuandikwa katika misingi ya kulinda kundi fulani na kugandamiza jingine.

Alisema kuwa hali hiyo ilianza kujionesha wakati wa utoaji maoni ya wadau katika muswada wa sheria ya kusimamia uratibu wa uandikwaji katiba mpya, akisema kuwa kama mchakato huo muhimu kwa maslahi ya nchi utachukua mwelekeo huo utakuwa 'mguu si sahihi'.

"Ukiwa wewe ni kiongozi ambaye uko kwenye kambi ya upinzani unasema unaandika katiba ili umtoe aliyeko madarakani tayari unaanza na mguu ambao si sahihi. Lengo la katiba si wewe mpinzani ikusaidie kumtoa aliye madarakani.

"Na wewe uliyeko madarakani ukisema tunaandika katiba ili sisi tuendelee kubaki madarakani na yule jamaa wa pembeni asiweze kufaulu hata siku moja kuingia hapa, umeshatuingiza kwenye matatizo makubwa tayari. Katiba haitakiwi kumgandamiza mtu mmoja na kumsaidia mwingine.

"Tunashukuru kuwa mswada sasa umerudishwa. Tunaomba tunaohusika tuutengeneze kwa nia njema, uadilifu, umakini na kwa maslahi mapana ya taifa letu. Tukitaka kutengeneza mswada kwa ajili ya kulinda maslahi ya vikundi au matabaka fulani ya watu, historia haitatusamehe," alisema Askofu Nzigilwa.

Aliongeza kuwa si vyema wote wanaohusika wakaingiza hila na udanganyifu katika mchakato muhimu kama huo kwa taifa taifa, akisihi Watanzania wote washiriki katika shughuli hiyo wakiongozwa na uadilifu, nia safi kwa maslahi ya taifa zima.

Askofu Nzigilwa alisema pia kuwa si vyema kuachana na kila kitu kilichoko katika katiba ya sasa, akisema kuwa haikuwa kitabu cha shetani, wala si mbaya kiasi inavyosemwa, kwani bado baadhi ya vitu vilivyomo ni vizuri, akiwataka Watanzania kuamua kuyabakiza na kuyaendeleza.

Kisha akaonekana kuzungumzia kwa lugha ya kifasihi kwa kutoa mfano kutoka katika biblia alisema si vyema katika mchakato wa utoaji wa maoni ya katiba mpya, watu wakazuiwa kuzungumzia baadhi ya mambo, akisema kuwa Watanzania waachwe waguse kila sehemu, almuradi waendelee kuishi kwa furaha, amani na mshikamano.

"Katika mjadala huu wa kupata katiba mpya tusiwekewe mti wa katikati, katika biblia katika ile Bustani ya Edeni, Mungu aliwaambia Adam na Eva, Mungu aliwaruhusu guseni kila mahali lakini isipokuwa ule mti wa katikati, kwa maana kwamba ule mti ulikuwa mbaya, pana hatari.

"Katiba yetu ya sasa ina mambo mema mengi tu, ambayo Watanzania tunaweza kugusa kila sehemu, popote na bado tukaendelea kuishi kwa amani, furaha na mshikamano, ilimuradi tuongozwe na nia njema, kwa usafi, tukiomba neema na baraka za Mwenyezi Mungu zituongoze katika hilo, sina wasiwasi katiba mpya nzuri tutaipata".

Mambo hayo ambayo Askofu Nzigilwa alionekana kuyazungumzia yalitajwa katika kipengele cha 9(2) cha muswada wa sheria ya marejeo ya katiba uliowasilishwa hivi bungeni kabla haujarudishwa serikalini kubadilishwa.

Kifungu hicho katika sehemu ya tatu ya muswada huo, kinataja mambo manane ambayo yalielezwa kuwa ni marufuku watu kuyahoji au kuyazungumzia wakati tume ya kukusanya maoni ya watu juu ya katiba mpya itakapokuwa ikitekeleza majukumu yake.

Masuala hayo yanayoitwa kuwa ya 'heshima na utukufu', hivyo hayapaswi kuguswa kwa maslahi ya taifa, yalikuwa yameainishwa katika muswada huo kama ifuatavyo; Kuwepo kwa Muungano wa Tanzania na Zanzibar, kuwepo kwa mihimili mitatu ya dola (bunge, serikali na mahakama), nafasi ya urais, mshikamano wa kitaifa na amani ya nchi.

Mengine ni; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwepo kwa mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia, haki za binadamu, dhana ya utu wa mtu, usawa mbele ya sheria na mfumo unaoweka utaratibu wa kufuata sheria, dhana ya Serikali ya Tanzania kutokuwa na dini na uhuru wa mahakama.

7 comments:

  1. BRAVOO ASKOFU HAYO NDIO MANENO YA BUSARA TUNAYO YATAKA. WANASIASA WASITEKE HILI LA KATIBA KWANI WAO SIASA WAMEIGEUZA KUWA BIASHARA NA HULKA YA MFANYABIASHARA NI KUPATA FAIDA NA BIASHARA YAKE

    ReplyDelete
  2. Safi sana,vijibwa vya Slaa viko kimya,umewapenya? au hamjalipwa posho?

    ReplyDelete
  3. ANONYMOUS SAID,CHANGIA HOJA SIO KUSEMA MANENO YASIYO MAZURI KWA JAMII,IKIWA KILA MTU ANA HAKI YA KUTOA MAONI YAKE NDUGU YANGU USIFANYE HIVYO TENA,TUBADILIKE CHANGIA HOJA

    ReplyDelete
  4. Pamoja na uhuru wa kutoa maoni, lakini hatuna budi kuwa na mipaka. Ukiwa mtu wa kukurupuka ni aibu, posho gani inayosema mchangiaji wa 2 hapo juu?

    ReplyDelete
  5. EWE MUUMBA MWENYEEZI MUNGU TUNAKUOMBA UWAJAALIE HAO WASIO NA KIPATO WAPATE, NA WASIO NA BUSARA UWAPE BUSARA NA PIA WABADILIKE WAWE WEMA KTK JAMII,HAKIKA INASIKITISHA MTU BADALA YA KUTOA MAONI AU MCHANGO WENYE FAIDA KWA JAMII ANAONYESHA WEREVU WAKE ILIMRADI AWEKE UOVU WAKE TUWE WASTAARABU

    ReplyDelete
  6. NIA NA MADHUMUNI YA KUWAOMBEA DUA HAO WATU NI KUKOSA AJIRA NA SHUGHULI YA KUWASHUGHULISHA MATOKEO YAKE NI KUTOA MCHANGO AU MAONI YASIYO NA TIJA HAYA YOTE NI KUKOSA KAZI YA KUFANYA NA KUFUKIRI

    ReplyDelete
  7. we anony huna mamlaka ya kumwita mwenzio KIJIBWA..mambo hayo ni ya kwenu huko huko CCM...

    haya rudini serekalini mkasimamie kutoa muswada mpya wa mchakato...na usiwe na maudhui ya kumlindeni mlio madarakani.

    ReplyDelete