LONDON, England
KOCHA wa Chelsea, Carlo Ancelotti anaamini siku 14 zijazo ndiyo zitakuwa kipindi kigumu wakati mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, zitakapokuwa zimeingia
katika mwezi wa mwisho.
Hivi sasa kikosi hicho cha Stamford Bridge, ambacho kilikuwa hakifanyi vizuri kwa sasa ndiyo kinaonekana kuwa mpinzani mkubwa wa Manchester United, baada ya kushuhudiwa Arsenal Jumapili ikifungwa na Bolton na kikosi hicho kitakutana na cha Sir Alex Ferguson Mei 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Mabingwa hao watetezi wanaamini kuwa wapinzani wao Arsenal, mwishoni mwa wiki hii wanaweza kuwapa hafueni wakati Manchester United itakapofunga safari hadi kwenye Uwanja wa Emirates ikisaka kuendelea kukaa kileleni kwa pointi nne.
Wakati Man United ikisaka pointi tatu kwa Arsenal, Chelsea wao watakuwa wakikabiliana na wapinzani wa Gunners katika ukanda wa Kaskazini mwa jiji la London, Tottenham siku moja kabla.
Akizungumzia kuhusu ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya West Ham, Ancelotti alisema: “Endapo tutaweza kuifunga Tottenham, tutaweza kuipa presha Manchester United wakati wa mechi dhidi ya Arsenal.
“Tuna mechi mbili muhimu. Ubingwa utaamuliwa ndani ya siku 14,” aliongeza.
Mbali na kupigia mahesabu ubingwa huo ndani ya siku 14, Ancelotti pia alipuuza kuwepo kwa uwezekano wa ubingwa kuamuliwa kwa tofauti ya magoli, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu Arsenal ilipoipiku Liverpool mwaka 1989.
Akizungumzia kuhusu kuwepo kwa uwezekano huo, kocha huyo alisema kuwa “Inaweza kutokea, hivyo jambo la muhimu tunahitaji kufunga mabao matatu na leo hatukustahili kufunga mabao matatu, lakini ni vizuri."
Kocha huyo wa zamani wa timu ya AC Milan, pia alisema kikosi chake hakiwezi kujizuia kupoteza pointi moja hadi mwishoni mwa msimu na akasema pia mechi dhidi ya Everton na Newcastle, ndizo zitakazotoa mwelekeo.
“Itakuwa vigumu kushinda mechi zote nne, tunakabiliwa na mechi ngumu," alisema. "Tunafahamu kwamba endapo tutapoteza mechi moja tutakuwa tumepoteza matumaini yetu na hapo ndipo itakapoanza presha,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment