Na Tumaini Makene
JUMLA ya shule za msingi 150 katika wilaya 17 nchini zimenufaika na mradi wa majaribio wa Elimu kwa Teknolojia, uliofadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa
Marekani (USAID), ambapo mitaala ya baadhi ya masomo inafundishwa kwa njia ya picha za video.
Mradi huo wa majaribio ulioanza mwaka 2008, kupitia Shirika la Tanzania Youth Foundation, huku Wizara ya Elimu na Mafunzo Stadi ikiwa ni mshirika mkuu, ulilenga kutumia teknolojia katika kuboresha ufundishaji na elimu kwa ujumla, hususan kwa shule za msingi.
Kwa mujibu wa Bi. Zamaradi Saidi, Mtaalamu wa Elimu na Mafundisho kutoka Tanzania Youth Foundation alisema kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kuendesha mradi wa namna hiyo, huku duniani ikiwa ni ya pili, baada ya nchi ya Philipine.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Bagamoyo katika warsha ya kuwapatia uwezo watumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo Stadi, ili kundeleza mradi huo utakapokabidhiwa rasmi kwa serikali Desemba mwaka huu, Bi. Saidi alisema kuwa mradi huo ni fursa muhimu ya kuboresha elimu nchini kwani inamsaidia mwanafunzi kuelewa kwa kusikia na kuona.
"Nia ya mradi huu wa majaribio wa Elimu kwa Teknolojia, ulikuwa na lengo la ku-demonstrate na kuonesha wizara kuwa inaweza kutumia teknolojia katika kufundisha kwa kuingiza mitaala ya shule katika hali ya picha ya video, kisha kwa kutumia simu ya mkononi aina ya Nokia N95 mwalimu anaweza kuchukua video hizo kwa kutumia mtandao wa Vodacom.
"Kwa hiyo USAID kwa kushirikiana na Vodacom, Pearson Foundation, Wizara ya Elimu na Mafunzo Stadi kama mdau mkuu pamoja na Tanzania Youth Foundation tuligawa screen kubwa za tv, simu hiyo ya Nokia pamoja na vifaa vyake vyote kama cables kumrahisishia mwalimu ku-download mitaala hiyo ya Tanzania ambayo imebadilishwa na kuwekwa katika video.
"Tulichofanya ni kuchukua mtaala wa Tanzania na kuuweka katika teknolojia ya video, lengo likiwa ni kuboresha ufundishaji na kujifunza...pia tumewafundisha walimu mbinu shirikishi katika kuwafundisha wanafunzi, kwani lengo sasa ni kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakuwa mshiriki mkuu katika kujifunza, si kusikiliza tu," alisema Bi. Saidi.
Alisema kuwa mara mradi utakapokabidhiwa, serikali inalo jukumu la kupanua wigo kwa maana ya kuongeza idadi ya masomo kutoka mawili ya sasa, hisabati na sayansi pekee, kupanua idadi ya madarasa, kwani majaribio yalifanywa kwa wanafunzi wa darasa la tano na sita.
"Wanayo nafasi ya kupanua wigo, wanaweza kuongeza madarasa, wakaongeza masomo, wakaongeza ikawa sasa ni ya nchi nzima badala ya mikoa mitano, wilaya 17 na shule 150 tulizofanya katika mradi wa majaribio, ili fursa hii iwafikie watoto wengi zaidi nchini wanufaike kama walivyonufaika kule tulikofanya," alisema Bi. Saidi.
Kwa upande wake, mratibu wa mradi huo kutoka wizarani, Bw. Jumanne Shauri alisema kuwa mradi huo ni mzuri ukitoa changamoto kwa sera ya wizara hiyo kufundisha kwa kutumia teknolojia ya habari na mwasiliano katika ufundishaji na kujifunza, ikiongeza ufanisi katika zana za chaki na mbao, ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu kufundishia.
Alisema kuwa mradi huo utaboreshwa zaidi katika bajeti ijayo ya wizara hiyo kwa kupangiwa fungu, lakini hasa kwa kuwekwa katika mkakati mkubwa wa 'Tanzania beyond tommorow', ambao umelenga kutumia matumizi ya teknolojia kwa kiasia kikubwa katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Naye mmoja wa wakaguzi wa elimu kutoka Wilaya ya Temeke, Bi. Teophlida Mwinyikambi, ambaye alikuwa mmoja wa waliopewa mafunzo ya namna ya kukagua mradi huo mara utakapokuwa chini ya serikali, alisema kuwa mradi huo una tija kwa wanafunzi na walimu, kwani mafunzo kwa televisheni yanamfanya mfundishaji kuzungumza kidogo, huku mfundishwaji akielewa zaidi kwa kuona na kusikiliza picha.
Aliongeza kuwa wakaguzi wameelekezwa namna ambavyo watakuwa wakikagua mradi huo, hasa katika maeneo ya mbinu za ufundishaji ambazo walimu watakuwa wanatumia, huku akisema katika maeneo ya mradi huo, mahudhurio ya wanafunzi shuleni yameonekana kuongezeka.
No comments:
Post a Comment