Na Israel Mwaisaka, Kyela
JESHI la Polisi wilayani Kyela jana lilitumia mabomu ya machozi na risasi za moto kwa lengo la kuwatanya wananchi walioandamana hadi Mahakama ya Wilaya hiyo
wakitaka kumshinikiza kuachiwa huru watuhumiwa 12 waliofikishwa mahakamani hapo kwa makosa mbalimbali.
Wananchi hao kutoka Kijiji cha Njisi Kata ya Katumba Songwe, walianza kuwasili katika viwanja vya mahakama kuanzia saa 1:00 asubuhi wakitumia usafiri wa baiskeli na wengine kwa miguu na mara hadi likawa kundi linalokadiriwa kufikia watu 3,000, na kuanza kujipanga kuingia lango kuu la mahakama hiyo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema kwamba mara baada ya kuwasili kwa wananchi hao, walikuwa na matumaini makubwa ya kuwawekea dhamana wenzao 12 waliofikishwa katika mahakama hiyo, wakituhumiwa kuvunja nyumba, kuiba sh. 1.6 pamoja na kuichoma moto nyumba hiyo.
Matumaini ya wananchi hao yalififia pale Hakimu wa Mahakama hiyo ya wilaya, Bw. Joseph Lwambano, alipoahirisha kesi hiyo hadi Aprili 11, mwaka huu itakapotajwa tena huku washitakiwa wakinyimwa dhamana kwa kilichodaiwa kukosekana kwa usalama, hatua ambayo iliamsha hasira za wazi kutoka kwa wananchi hao.
Baada ya hakimu kuahirisha kesi hiyo wananchi hao walilizuia gari la polisi aina ya land rover lenye namba PT:0798 lililowabeba watuhumiwa kuwapelekea mahabusu, Tukuyu wilayani Rungwe, na kutaka kuwashusha watuhumiwa kwa nguvu.
Wakati huo wananchi hao walikuwa wakiimba 'Tumechoshwa na wachawi! Tumechoshwa na wachawi!
Kutokana na hali hiyo polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi baridi ili kuwatawanya wananchi waliokuwa na hasira, jambo ambalo lilisababisha mapigano makali kutokea kati ya wananchi hao waliokuwa wakirusha mawe kwa askari polisi.
Mapigano hayo yalidumu kwa saa tatu, na kusababisha polisi kuwashikilia watu wanane, wakiwemo wanawake wanne wakihusishwa na ghasia hizo.
wananchi wenzangu wa kyela tuwe watulivu na tuache sheria ichukue mkondo wake. huo ndio ustaarabu na msingi wa utawala bora!
ReplyDelete