Na Peter Mwenda
WATU walioathirika na mlipuko wa mabomu ya Gongalamboto na kutibiwa katika kituo cha Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) cha Mazizini Ukonga
wamefikia 1,204, kati yao 150 walikuwa na msongo wa mawazo.
Kamanda wa Kituo hicho, Meja Pius Horumpende alisema wagonjwa hao ni wale waliopatwa na mshituko wa mabomu yaliyolipuka katika kambi ya JTWZ kambi ya Gongolamboto Februari 16 mwaka huu.
Dkt. Horumpende alisema siku saba za mwanzo kituo hicho kilipokea wagonjwa 749 ambao ni sawa na wastani wa wagonjwa 107 kwa siku wakiumwa magonjwa mbalimbali yaliyotokana na mabomu.
"Tumepokea wagonjwa waliookuwa wanaumwa vifua, kuumwa kichwa, masikio kuuma, macho kutoa machozi, msongo wa mawazo yaani mgonjwa kujikuta anaota njozi za kutisha, shinikizo la damu, kuhara na magonjwa ya ngozi," alisema Dkt. Horumpende.
Alisema kituo pia kinatoa tiba kwa wagonjwa wengine ambao hawakudhurika na mlipuko huo katika eneo la Mazizini katika kata za Ukonga na Kata nyingine za jirani za Kitunda, Kivule na Majohe.
Hata hivyo, alisema kuwa huduma hiyo wengine wanaichukulia vibaya kwani baadhi ya wananchi wasio waaminifu wanaotuma watoto wao kusingizia kuwa wagonjwa ili wapate dawa.
Dkt. Horumpende alisema kutokana na mlipuko huo anaishauri Serikali kuweka kitengo cha ushauri nasaha kwa ajili ya matukio ya kushtukiza yanayosababisha msongo wa mawazo.
"Hata wafungwa wanapomaliza kifungo chao wanapaswa kupata ushauri ili asiathirike kiakili na kurudia makosa waliyofanya awali, ili wasirudi tena gerezani," alisema Dkt. Horumpende.
Alisema huduma za matibabu zinaendelea kutolewa bure na kituo hicho kinaendelea kuwahudumia wagonjwa wakati wowote hadi watakapopungua.
No comments:
Post a Comment