24 April 2011

Kigogo CCM ataka Ofisi za seriksli zihamishwe

Na Yusuph Mussa, Same

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same Bw. August Kessy ametaka
ofisi zote za Serikali za watendaji wa vijiji na kata kwenye wilaya hiyo
 kuhama kwenye majengo ya CCM.

Akizungumza wiki hii kwenye Baraza la Madiwani la Bajeti la Halmashauri hiyo alisema majengo hayo ni mali ya CCM, hivyo imefika wakati wa halmashauri kujenga ofisi zake badala ya kutumia hizo za CCM.
“Tunataka ofisi za vijiji na kata ziondoke kwenye majengo ya CCM na badala yake
halmashauri ijenge majengo yake kila kijiji na kata, hiyo ni kutaka kufanya mali za
CCM zijulikane” alisema Bw. Kessy.

Pamoja na hilo, Bw. Kessy ameitaka halmashauri hiyo kutoa mrejesho wa kila
inachokifanya kwenye wilaya hiyo hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo, huku
akisisitiza hakuna Idara ya Halmashauri ambayo itafikia malengo yake bila
kukishirikisha chama.
“Tunataka kila baada ya muda tuweze kuelewa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye
Halmashauri, lengo ni kutaka kuona kila mradi ulivyokadiriwa fedha zake unakamilika.
Pia tunataka kila Idara ya Halmashauri inashirikiana na chama kuona inafanikisha
miradi yake... Idara isiyokwenda sambamba na chama kamwe haiwezi kufikia malengo
yake,” alisema Bw. Kessy.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
hiyo Bw. Joseph Mkude alisema chama kimewaweka majaribuni kwa kutaka kuwanyang’anya ofisi kwenye vijiji, kwani wana uwezo wa kujenga za kwao, lakini sio katika kasi hiyo aliyobainisha Bw. Kessy.
“Kwa kweli Mwenyekiti ametuweka majaribuni. Ngoja tuone, ikiwa Korogwe (akiwa Afisa
Mipango wa Wilaya) nimeweza kujenga kila kata katika kata 16 Ofisi ya Mtendaji Kata,
hata huku siwezi kushindwa kufanya hivyo, ni mipango tu” alisema Bw. Mkude.
Hata hivyo mmoja wa madiwani ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, alihoji ni
vipi CCM inakuwa na mashaka na mali zake wakati huu, kuna dalili gani inaziona kuwa
siku moja huenda Serikali ikaongozwa na chama kingine hivyo ikapoteza mali zake, ama
ikakaribisha watendaji wa vyama vya upinzani kwenye ofisi hizo?.

No comments:

Post a Comment