Na Mwandishi Wetu, Handeni
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, wametoa karipio kali kwa watumishi wa Idara ya Ardhi, kwa madai kuwa wamekuwa na urasimu
mkubwa katika utendaji wao wa
kazi na kwamba wamekuwa wakionesha nidhamu mbaya kwa wawakilishi hao wa wananchi.
Idara hiyo pia imelalamikiwa kwamba imekuwa ikitoa hati za kumiliki ardhi maeneo
makubwa kwa watu binafsi kiholela, bila kushirikisha Serikali za vijiji kupitia
mikutano halali.
Karipio hilo walilitoa jana katika kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya
wilaya hiyo maarufu kwa jina la Ufungilo, kilichofanyika mjini Chanika.
"Baraza hili la madiwani linatoa karipio kali kwa Idara ya Ardhi, kwa kushindwa
kuonyesha ufanisi wa kazi zake. Hawana nidhamu kwa madiwani, wanafanya kazi zao
chini ya kasi tuliokuwa tukiitarajia, urasimu umezidi katika idara hii. Mtuelewe kwamba sisi hatuja taja jina la mtu, ila tunalalamikia idara hii. Tunakuagiza
Mkurugenzi ufuatilie ili kuondoa mapungufu haya," alisema Mwenyekiti wa Halmashauri
ya wilaya hiyo Bw. Ramadhani Diriwa alipokuwa akiahirisha kikao hicho.
Diwani wa Kata ya Ndolwa Bw. Joel Mabula alisema kuwa, kuna migogoro mingi ya ardhi
wilayani hapa, na kuitaja kuwa ni pamoja na vijiji vya Nkale, Chanika kofi, Seza
kofi, Mumbwi, Kwedichocho, Mazingara, Komfungo na Kwamnele. Kwamba idara hiyo
imekuwa na urasimu mkubwa kushughurikia migogoro hiyo.
Idara nyingine iliyolalamikiwa ni Idaya ya Mipango, ambayo imedaiwa kuwa nayo
imekithiri kwa urasimu. Kwamba imekuwa ikichelewesha kupeleka fedha za ruzuku
vijijini.
Diwani wa kata ya Mazingara Bw. Yahaya Kijori alisema kuwa, urasimu unaoendelea
katika idara ya Mipango usipodhibitiwa, utasababisha hasara kubwa katika kuleta
maendeleo vijijini.
"Ofisi hii ya mipango ina urasimu wa kutoidhinisha fedha za maendeleo kwa wakati.
Tatizo hili ni kubwa mno kamati za maendeleo ya vijiji zinatumia gharama kubwa ya
ufuatiliaji wilayani, wajua mimi sizungumzi kwaajili ya matatizo ya vijiji vilivyopo
katika kata yangu ya mazingara, ila tatizo hilo ni kwa Wilaya nzima" alisema Bw.
Kijori na kuongeza kuwa.
"Miradi mingi inayoibuliwa kule vijijini mingi huwa inarudishwa, sasa imekuwa
ikiibuliwa miradi mbalimbali kutokana na maelekezo, ya Serikali, lakini kasi ya
utekelezaji ni ndogo. Urasimu huo unasababisha matumizi makubwa gharama za
ufuatiliaji kwa vikundi hivyo" alisema.
Naye Afisa Mipango wilayani hapa Bw. Dawson Temu akijibu tuhuma hizo, alikiri kuwepo
na urasimu huo na kusema kuwa, inatokana na fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali
kuu kutofika wilayani kwa wakati.
No comments:
Post a Comment