04 April 2011

Migiro, Kikwete wamlilia Lusekelo

Mwandishi Wetu

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Asha-Rose Migiro ameelezea kusikitishwa kwake na kifo cha mwandishi wa habari nguli, Bw. Adam Lusekelo aliyefariki
dunia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Naibu Katibu Mkuu alieleza kusikitishwa na kifo hicho kupitia taarifa aliyoitoa jana kwenye vyombo vya habari akieleza kuwa alizipokea taarifa za kifo cha Bw. Lusekelo kwa majonzi makubwa.

"Alikuwa mwandishi mwenye kipaji kikubwa na mwandishi mahiri, alikuwa na uwezo wa kuieleza jamii kuhusu mambo ya kijamii kwa njia fasaha wakati akigusa maisha ya watu wa kawaida," alisema.

Dkt. Migiro alisema kuwa alianza kusoma makala za  Bw. Lusekelo tangu akiwa Chuo Kikuu na amekuwa akiendelea kuzisoma hadi sasa, huku akiwashukuru marafiki zake ambao walikuwa wakifahamu mapenzi yake kwa makala  za Bw. Lusekelo, ambao walikuwa wakihakikisha anapata makala hizo.

"'Nitaimisi' kalamu Adamu! kifo chake ni pigo kubwa  kwa familia yake na marafiki zake wengi. Ni hasara kubwa kwa ndugu wa vyombo vya habari na Tanzania kwa ujumla. Maombi yangu na rambirambi ziiendee familia yake katika wakati huu wa huzuni," alisema Dkt. Migiro.

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za sambirambi kutokana na kifo cha Bw. Lusekelo kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete alisema alimfahamu vema Bw. Lusekelo kwa jitihada zake kubwa za kuendeleza taaluma ya tandishi wa habari kwa kuandikia magazeti mbalimbali hapa nchini yakiwemo ya Serikali ya Daily News na Habari Leo.

“Ninamkumbuka zaidi Marehemu Lusekelo kwa safu yake maafuru ya “The Light Touch” iliyokuwa na mafundisho muhimu kwa jamii yetu”, alisema Rais Kikwete na kuongeza, “Kifo cha Marehemu Adam Lusekelo ni pigo kubwa kwa Taaluma ya Uandishi wa Habari na wanahabari wenyewe hapa nchini, na kimeacha pengo kubwa katika taaluma hiyo ambalo si rahisi kuzibika”.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete ametoa pole kwa familia ya marehemu Lusekelo kutokana na kuondokewa na mpendwa wao ambaye amesema alikuwa mhimili madhubuti na tegemeo kubwa kwa ustawi wa familia.

1 comment:

  1. He was a journalist of the highest calibre. He was a philosopher in his own right.Fearlessly independent, very professional, analytical,decisive and socially conscious.

    I MISS YOU ADAM.

    May the Lord Rest YOU in PEACE. Amen

    ReplyDelete