Na Mohamed Akida
UONGOZI wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, umepanga kusajili kikosi cha wachezaji 27 kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.Katibu Mkuu wa
klabu hiyo, Mwesigwa Celestine, alisema mapendekezo hayo yametokana na ripoti iliyoachwa na Kocha Mkuu, Sam Timbe, aliyekwenda Uganda kwa mapunziko, baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu.
"Kocha amesema usajili wetu wa msimu ujao uwe na wachezaji 26 au 27, akiwa na maana wapya wawe nane au tisa,” alisema.
Kuhusu wachezaji wa nje, Mwesingwa alisema Kocha Timbe, ameamua kuendelea na wachezaji wawili, kipa Yerw Berko na Mzambia Davis Mwape.
Kwa uamuzi huo, wachezaji Isaack Boakye, Ernest Boakye na kipa raia wa Serbia, Ivan Knevezic hawataongezewa mkataba.
Katibu huyo alisema kuwa, nafasi hizo zilizoachwa na wachezaji wa nje, zitajazwa na mchezaji yeyote mwenye kiwango wa ndani, lakini kama kocha atampata mwingine, watamsajili.
Katibu huyo alisema kwa mujibu wa maagizo aliyoacha kocha Timbe, wachezaji watakaoachwa ni watatu, lakini wengine wanaweza kupelekwa kwa mkopo kwenye timu nyingine za Ligi Kuu Bara.
"Kocha alisema hana mpango wa kumtema mchezaji mwenye mkataba, na malengo yake ni kuwapeleka kwa mkopo kwenye timu nyingine ili wakakuze viwango vyao na kurejea kuitumikia timu yetu,"alisema.
Yanga baada ya kutwaa ubingwa wa Bara, wanajiimarisha katika usajili kwa ajili ya michuano ya kimataifa na ligi kuu msimu ujao.
No comments:
Post a Comment