18 April 2011

Kikwete aombwa kugeukia ufisadi Wizara ya Ujenzi

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete ameshauriwa kuvalia njuga mafisadi waliohusika na uuzaji nyumba za serikali kiholela bila kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na waliozigawa kwa
watu wasiostahili.

Rai hiyo ilitolewa jana na baadhi ya maofisa wa Wizara ya Ujenzi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, kupongeza hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, kutangaza vita ya ufisadi ndani ya chama hicho.

Hivi karibuni CCM ilitoa siku 90 kwa viongozi wake wanaohusishwa na kashfa mbalimbali za ufisadi ikiwemo Richmond, Kagoda, Dowans na ile ya Rada, kuachia ngazi kama hatua mojawapo ya kukisafisha chama hicho ambacho umaarufu wake umeshuka kwa kasi ndani ya jamii.

Maofisa hao ambao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina gazetini, walisema uamuzi huo unastahili kuungwa mkono na wapenda maendeleo wote nchini bila kujali itikadi zao.

Hata hivyo, mmoja wa vigogo hao alisema pamoja na hatua hiyo njema, Rais Kikwete bado ana kazi nzito kuutokomeza ufisadi katika sekta zote na kumtaka kutupia macho na kuwawajibisha mafisadi wote waliohusika na uuzaji nyumba za serikali kiholela bila kufuata taratibu na kuwagawia watu wasiostahili.

"Rais Kikwete sasa awashughulikie waliouza nyumba za serikali kiholela kwa maslahi binafsi. Nyumba nyingine tunajua ziligawiwa kwa mahawara. Wapo pia wanaoigombanisha serikali na wananchi na wanaoihujumu kwa makusudi kwa malengo ya kujipanga kuwania urais 2015," alisema mmoja wa vigogo hao.

Pamoja na kutomtaja jina, kauli ya maofisa hao inaonekana kumlenga moja kwa moja Waziri wa Ujenzi, Bw. John Magufuli, ambaye akiwa waziri wa wizara hiyo katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alisimamia utekelezaji wa sera hiyo inayoendelea kulalamikiwa na wananchi wengi hadi sasa, sambamba na ubabe wa bomoabomoa kwenye upanuzi wa barabara.

Hata hivyo kigogo huyo alibainisha kuwa Bw. Magufuli ameshindwa kutambua mwongozo wa serikali unaotumika kubomoa nyumba wa Februari 2009 (Road Sector Compensation and Resettlement Guideline) bila sababu za msingi, mwongozo ambao Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda walitumia kuzuia bomoabomoa ya kiholela.

"Inaelekea (Magufuli) hataki mwongoza huo kwa kuwa unamzuia kutumia ubabe na kwamba unamtaka kufidia wanaostahili kabla hawajabomolewa nyumba zao. Hatujui ni kwa lengo gani anakataa na kugombanisha serikali na wananchi," alidai kigogo huyo ambaye ni miongoni wa wahandisi wa wizara hiyo.

Mbali na hayo ufisadi mwingine unaodaiwa kuwepo Wizara ya Ujenzi ni suala la ukiukwaji taratibu za Sheria ya Manunuzi katika miradi ya barabara kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na kuisababishia hasara serikali.

"Sasa awashughulikie walioisababishia hasara serikali kutokana na ukiukwaji taratibu katika zabuni za barabara na sasa uchakachuaji wa uteuzi wa maofisa watendaji wakuu wa asasi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ikiwemo Tanroads, Temesa na idara zingine ndani ya wizara kwa maslahi binafsi," alisema.

Imedaiwa kuwa zimekuwepo pia jitihada za maksudi za uongozi wa wizara kuvuruga mchakato wa kumpata Mtendaji Mkuu wa Tanroads kwa kumpigia debe anayekaimu nafasi hiyo, Bw. Patrick Mfugale pamoja na kuwa kipindi alichotakiwa kukaimu kimepita.

"Tunajua alimteua Mfugale kukaimu nafasi hiyo kibabe bila kuufanyia upembuzi yakinifu uteuzi huo, hili si jambo jema, "alisema.

1 comment:

  1. SOPHIA SIMBA KATIKA KUTOMBOKA KWAKE ALISHAWAASA WATANZANIA KWAMBA HAKUNA MSAFI NDANI YA CCM! SASA MLIMWONA MSEMA OVYO LAKINI KAULI YAKE INA UKWELI. SEMENI. CHADEMA HOYEEEEE!

    ReplyDelete