Na Heri Shaaban
JAJI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhan ameibua udhaifu mwingine kwenye katiba ya sasa katika kipengele cha Rais wa Zanzibar kuwa mjumbe wa Baraza la
Mawaziri la Jamhuri ya Muungano, kuwa ipo siku kitazua utata mkubwa.
Alisema kwa sasa inaonekana kama si tatizo kwa kuwa wote wanatoka chama kimoja, lakini ikiwa chama tofauti kitaingia madarakani upande wowote, itakuwa jambo la ajabu kwa Rais huyo kuingia kwenye baraza hilo.
Jaji Ramadhani alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam juzi katika mahojiano maalumu yaliyorushwa na Kituo cha Televisheni ya ITV wakati akielezea changamoto mbalimbali zinazokabili mahakama nchini.
Alisema kuwa mapungufu katika katiba hiyo ni mengi, ingawa wananchi wengi hawaifahamu vyema katiba ya sasa.
"Wananchi watoe maoni yao tuangalie itakavyokuwa, hakuna haja ya kuwepo malumbano na kuvuruga amani iliyopo nchini, na ndiyo maana serikali imeamua kuwashirikisha wananchi waweze kutoa maoni yao," alisema Jaji Ramadhan.
Bw. Ramadhani alisema hata kwa upande wa majaji wa Mahakama Kuu katiba iliyopo inawabana katika umri kustaafu kuwa miaka 60, huku akihoji kwa nini isiwe 65 kama ilivyo kwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.
Hata hivyo, hakutaka kuingia kwa undani kuhumu muswada huo, hasa eneo la mgawanyo wa madaraka ya dola, mahakama na bunge, akisema anayo nafasi yake maalumu ya kutoa maoni, badala ya kuyatoa hadharani yakawavuruga wananchi.
Kuhusu utendaji wa mahakama, alisema kuwa wananchi wasiisibebeshe lawama za kuchelewesha kesi, kwa kuwa suala la upelelezi linasimamiwa na Jeshi la Polisi si mahakama, na hakimu au jaji hulazimika kusikiliza pande zote wakati wa kusikiliza kesi.
"Mfano wakili au mwendesha mashtaka akisema amefiwa. Jaji au hakimu hawezi kusema tuendelee hata kama umefiwa, maana ipo siku hata yeye anaweza kufiwa," alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi wapatiwe elimu ya kutosha kwanza na si kubebesha lawama mahakama kwa kuwa kabla ya kufika mahakamani upelelezi unafanywa na polisi," alisema Ramadhani.
Alisema kwa sasa hataki kushughulika na maswala ya siasa badala yake anashughulika na mahakama ya Afrika mashariki kwa kuwa taaluma yake ni mwanasheria.
Tunakupongeza Jaji mstaafu, muhimu kuwe na sheria kuhusu kesi za jinai au kesi yoyote isizidi miaka miwili ikipita hapo kesi ifutwe na hakuna kurudi tena mahakamani maana uchunguzi gani wa Polisi unachukuwa miaka zaidi ya 5 eti bado upelelezi haujakamilika ni mbinu za Rushwa na kumkanadamiza na kumkomoa mshtakiwa. ili kuharakisha hawa Polisi wafanye kazi zao haraka wapewe muda maalumu ikipita hapo ni kesi kufutwa.
ReplyDeleteJaji Mkuu Mstaafu kwa hili la viongozi wa vyama mbali mbali kuwa kwenye baraza moja la mawaziri ni jambo la kawaida tu kwenye mfumo wa vyama vingi.Tatizo unaloliona wewe ni dhana itokanayo na mfumo wa chama kimoja inayotawala hapa Tanzania, "the winner takes it all", ambayo si lazima na si njema katika utawala wa vyama vingi. Mfumo wa vyama vingi si uahini kati ya vyama!
ReplyDeleteIla la pili nitakalolesemea tu ni doa kubwa uliloacha katika mfumo wetu wa sheria, nalo si ucheleweshwaji wa kesi bali ile hukumu ya mgombea binafsi uliyoitoa pamoja na waheshimiwa majaji wengine 6. Kwa hakika uamuzi ule ulidhoofisha sana imani ya wananchi kwa muhimili wa mahakama, kama chombo huru! Hata sasa wanasiasa wengi wanaacha kupeleka kesi zao mahakamani si kwa sababu hawahisi wanakosewa haki, bali kwa sababu hawana imani na mahakama tena! Mfano mzuri ni vurugu zinazoendelea katika halmashauri ya jiji la Arusha. Wanasiasa wamekataa kupeleka malalamiko yao mahakamani kwa kuwa wnahisi haki haitatendeka! Hii ni dosari kubwa ya legacy yako uliyoiacha