Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa klabu ya Yanga umewapa motisha ya sh. milioni 20 wachezaji wake, baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mwaka 2011/2012.Yanga
ilicheza Jumapili iliyopita na Toto African ya Mwanza, na kuifunga mabao 3-0 na hivyo kuwazidi mahasimu wao Simba bao moja baada ya kulingana kwa pointi, ambapo kila moja ilikuwa na pointi 49, tofauti ikawa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga alisema fedha hizo ni tofauti na zile za ubingwa, ambapo Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na Kamati ya Mashindano zilichanga kiasi hicho kwa ajili ya kuwapa motisha wachezaji hao.
"Kazi waliyofanya wachezaji wetu ni kubwa, hivyo sisi kama viongozi tumeona ni vyema tukawapa motisha ili waweze kujituma hata katika michuano mingine inayokuja," alisema Nchunga.
Alisema katika fedha hizo, sh. milioni 7 tayari walishawapa wachezaji hao baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-1 na sh. milioni 13 zilizosalia watawakabidhi wiki hii.
Nchunga alisema kwa motisha hiyo waliyoitoa, wanaamini kabisa wachezaji hao wataendelea kujituma hata katika michuano ya kimataifa na hivyo kuendelea kuipa sifa klabu yao.
Mwenyekiti huyo alisema, pia wanaamini bado kuna mtu mmoja mmoja ambaye ambao watakuwa wameguswa na ubingwa huo na hivyo kuwazawadia wachezaji wao kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Kuhusu fedha za ubingwa, ambazo huwa zinatolewa na wadhamini Wakuu Kampuni ya simu za mkononi Vodacom, uongozi utaangalia bonasi ambayo wachezaji watatakiwa kupata, lakini kwa sasa hawawezi kusema lolote mpaka pale watakapokabidhiwa.
"Fedha ya ubingwa kuna utaratibu wake hivyo tunasubiri wadhamini wetu, Vodacom watukabidhi ili tuweze kupitia mkataba vizuri kwa ajili ya bonasi kwa wachezaji wetu," alisema.
No comments:
Post a Comment