18 April 2011

'Gamba la CCM' laivuruga Kahama

Na Patrick Mabula, Kahama

HALIMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Wilayani Kahama iliyokutana juzi kuupongeza uongozi wa juu wa chama hicho kwa 'kujivua gamba' na kuwatosa
baadhi ya viongozi wa taifa, walijikuta wakivurugana huku wengine wakishinikiza viongozi wa ngazi ya wilaya nao wajivue magamba na kujiuzulu.

Hali hiyo ilitokea baada ya CCM wilaya kuitisha Halmashauri Kuu Maalumu kwa lengo la kupongeza hatua iliyochukuliwa na chama hicho ngazi ya taifa ya kujivua magamba na kuwatosa baadhi ya viongozi wa ngazi ya taifa, ambako walijikutana wao kwa wao wakitakiwa kujivua magamba pia.

CCM wiki iliyopita iliwatosa baadhi ya vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi kwenye Kamati Kuu na kuwapata kupima wenyewe na kujiengua kwenye Halmashauri Kuu ndani ya siku 90, hatua ambayo imebaitizwa kama kujivua magamba.

Katika kikao hicho, wajumbe walianza kwa kurushiana maneno kuwa wamekuwa mabingwa wa kupongeza hatua za viongozi wa ngazi ya juu kukinusuru chama huku nao wakiwa na mapungufu mengi.

Kutokana na uamuzi huo ambao umeibua mjadala nchini, Mwenyekiti wa CCM wa Vijana Kata ya Kahama mjini, Bw. Mathias Misungwi aliwaeleza wajumbe wenzake kuwa kuupongeza uongozi wa juu kwa hatua waliyoichukua chini ya Rais Jakaya Kikwete ni sawa na kuwataka nao wajivue magamba na kujiuzulu.

Bw. Misungwi alisema viongozi wa ngazi ya Wilaya ya Kahama nao
wana mapungufu mengi kuanzia mwenyekiti, katibu, Katibu wa Uchumi, mipango na fedha, Katibu wa Itikadi na Uenezi, hivyo nao lazima wapime na kujivua magamba na kuachia ngazi.

Naye Mjumbe wa Uchumi na Fedha kutoka kata ya Bulungwa
aliyejitambulisha kwa jina moja la Bw. Kapaya alisema hatua zilizochukuliwa na Uongozi wa CCM taifa wa kuwatosa baadhi ya viongozi wake, lazima zishuke hadi chini badala ya kukaa na kupongeza huku, wengi wakiwa na mapungufu na walishakivuruga chama.

Akijibu hoja hizo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kahama,
Bw.Sospeter Nyigoti na Katibu wa Siasa na Uenezi, Bw. Mipawa Wanangolelwa kwa nyakati tofauti waliwataka wajumbe katika ngazi za kata waanze wao kujivua magamba na kujiuzulu.

Hata hivyo baadaye walielewana na kukubaliana kufanya maandamano kutoka katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kahama walipofanyia mkutano huo hadi viwanja vya Kadeco walikofanya mkutano wa hadhara.

Katika viwanja vya Kadeco kulikuwa na wasanii mbalimbali waliokuwa wamevuta watu lakini viongozi hao walipofika na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kahama, Bw. Andrew Masanje kupanda jukwaani na kuanza kutoa hotuba, wananchi walisambaa
huku wakirusha maneno ya kuwataka nao wajivue magamba.

3 comments:

  1. Wamejipambanua vizuri, kuwa CCM kirefu chake ni Chama Cha Magamba. Ndo maana yapo kila sehemu, Kitaifa yapo, kimkoa, kiwilaya, kikata hata vijijini yapo, ukiachilia mbali kwenye jumuiya zao.

    ReplyDelete
  2. Hapo juu ukiwa mpumbavu utakuwa hivyo, afadhali ukubali uwe mjinga, mana unayo nafasi ya kujifunza.

    ReplyDelete
  3. ccm imepotoka kwani waasisi wake hawapoa. Waliopo hawjui malengo na madhumuni ya chama hicho. Kosa kubwa walilofanya ni kukumbatia wafanyabiashara na kuwaacha wakulima na wafanyakazi pembeni. Ukiangalia dhana nzima ya chama hicho na yanayofanyika ndani yake havioani kabisa

    Bendera yake in alama ya jembe na nyundo. Ni nani anajua hizo alama na maana yake? wala hawana sababu kwa vile wamekiweka rehani kwa wafanyabiashara na wenye fedha chafu,

    Hivi chama kilichokuwa na nguvu kama ccm, kulikuwa na haja gani ya kutumia mabango ya mabilioni? au kwa vile walishazoea ten pasenti kuna watu walitaka kupata chao?

    Chama chenye mtaji hata vijijini hakikuwa na sababu ya kuzuzuka na mabango ya bei mbaya namna ile. Hiyo ni kazi ya vyama vichanga visivyojulikana.

    Viongozi wengi waliingia kwenye pay roll za wahindi, ndiko walikoiuza nchi, wanalipwa huku fedha za nchi zikitoroshwa,madawa ya kulevya ambayo wenye biashara hiyo wanajulikana lakini kwa vile watoa maamuzi wapo kwenye payroll za wenye pesa si rahisi biashara hiyo kuisha.

    Ninaamini kwamba si rahisi ccm kujisafisha, imechafuka sana. Hata hivyo hakuna haja ya kukata tamaa kwani watz ni wasahaulifu sana: wakiwatosa mafisadi, wakirudisha nyumaba za serikali na hata kuwakamata wafanyabiashara ya madawa ya kulevya wanaeweza anhalau wanajali

    ReplyDelete